Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba (Mb) ameeleza kuwa ukatili wa kijinsia ni kosa la jinai na kila mwanachi wa Tanzania ana haki na wajibu wa kuripoti matukio hayo ili kuhakikisha waathirika wanapatiwa ulinzi na haki inatendeka
Mhe. Katimba amesema hayo Januari 9, 2026 Mkoani Singida wakati wa uzinduzi wa Kliniki ya Huduma za Msaada wa Kisheria uliofanywa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb).
Ameeleza kuwa matukio ya ukatili yanaweza kuripotiwa katika vituo vya Polisi kupitia dawati la jinsia na watoto, Ofisi za Ustawi wa Jamii, Vituo vya afya na hospitali pamoja na Madawati ya Msaada wa Kisheria yaliyopo katika ngazi za Halmashauri.
“Serikali imeweka namba 116 kwaajili ya kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia hususan kwa watoto ambapo matumizi ya namba hii ni bure. Aidha Wizara kupitia Kituo cha Huduma Kwa Mteja imeweka namba 0262160360 kwaajili ya kuripoti matukio mbalimbali ya Kisheria ikiwemo ukatili” Amesema Mhe. Katimba
Vilevile amefafanua kuwa Ukatili wa Kijinsia ni kitendo au vitendo vya unyanyasaji au mateso anavyofanyiwa mtu kwa misingi ya jinsia yake na kusababisha madhara ya kimwili, Kihisia, Kisaikolojia au Kiuchumi.
