Featured Kitaifa

WAZIRI SANGU: WAUNGANISHENI VIJANA NA FURSA ZA AJIRA NDANI NA NJE YA NCHI

Written by Alex Sonna

 

 

Na: OWM – KAM, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amekitaka Kitengo cha Huduma za Ajira kuongeza juhudi katika kuwaunganisha vijana na fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

Aidha, amesema Kitengo hicho kinajukumu kubwa la kuwasaidia watafuta ajira na waajiri, hivyo kuwaunganisha na fursa hizo za ajira kutapunguza idadi ya watu wasio na kazi hususan vijana.

Amesema hayo leo Disemba 20, 2025, alipotembelea Kitengo cha Huduma za Ajira, Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuona shughuli zinazotekelezwa na kitengo hicho.

Vilevile, Mhe. Sangu ametaka kitengo hicho kuhakikisha kinawafahamisha wananchi hususan vijana kuhusu fursa za ajira ambazo Serikali imezitafuta ndani na nje ya nchi wanazipata kwa wakati.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo amehamasisha viongozi na maafisa wa kitengo hicho kuanzisha ‘App’ ambayo itawezesha vijana kuchangamkia fursa za ajira kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Ajira, Josephine Matiro amesema kitengo hicho kitaendelea kuratibu na kuimarisha mifumo ya utoaji na usimamizi wa huduma za ajira.

About the author

Alex Sonna