WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Lindi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika eneo la Ngongo mkoani Lindi na kusema kwamba huo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya kupanua fursa za elimu ya juu nchini.
“Uwekezaji huu ni utekelezaji wa vitendo wa nguzo ya pili ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika kujenga uwezo wa watu kifikra, kiubunifu, kufanya uchambuzi, kutatua changamoto, pamoja na kuwa na utaalamu na umahiri katika nyanja mbalimbali za maisha,” amesema.
Akizungumza na viongozi na mamia ya wananchi wa mkoa wa Lindi waliofika kushuhudia uzinduzi huo leo (Jumamosi, Desemba 20, 2025), Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuamua kutekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupanua huduma za elimu ya juu katika maeneo ya kimkakati kama vile Mkoa wa Lindi.
“Maono haya ni ya kwake mwenyewe Mheshimiwa Rais. Zilipotolewa fedha za mradi huu kwa vyuo vikuu kama vya Dar es Salaam na Mzumbe, alisema ujenzi uelekezwe katika kupeleka kampasi za vyuo vikuu kwenye mikoa yote ambayo haikuwa na vyuo vikuu.”
Amesema Mkoa wa Lindi, kama ilivyo kwa mikoa mingine ya Kusini mwa Tanzania una ardhi yenye rutuba, rasilimali watu na mazingira rafiki kwa kilimo cha kisasa na biashara ya mazao.
“Kampasi hii ya kilimo itasogeza huduma ya elimu karibu na wananchi wa Kanda ya Kusini na kuendeleza utafiti na ubunifu katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa letu. Uwekezaji huu utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo kupitia maarifa, teknolojia na tafiti za kisasa zitakazojibu changamoto halisi za wakulima wetu,” amesisitiza.
Dkt. Mwigulu amesema ujenzi wa Kampasi ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Lindi ni ushahidi mwingine wa dhamira ya dhati ya Serikali ya kuifanya elimu ya juu kuwa chombo cha mageuzi ya kiuchumi na kijamii. “Kupitia Kampasi hii, Serikali inalenga kuandaa wataalamu wabobezi wa kilimo, utafiti na biashara ya kilimo watakaosaidia kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao, ajira kwa vijana na mapato ya wakulima.”
Sambamba na ujenzi wa chuo hicho, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025, Serikali itahakikisha inafanya ukarabati wa barabara katika maeneo ya Nane Nane (Ngongo), ujenzi wa barabara zenye urefu wa km. sita kwa kiwango cha lami katika Kampasi za Chuo Kikuu (Ngongo na Ruangwa); ujenzi wa barabara za lami za Kilambo (km 1.5); Mtange – Kinengene – Kibaoni na barabara ya Mahakama – Mitwero (km 1.2).
Mapema, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete alimpongeza Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba kwa sababu yeye ni zao la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Shahada zako zote tatu umezipatia pale chuo kikuu. Tunajivunia kwani wewe ni miongoni mwa mabalozi wema wa chuo chetu,” alisema.
Akielezea uwekaji wa jiwe la msingi la Kampasi ya Lindi, Dkt. Kikwete alisema anaamini iko siku kampasi ya Lindi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nayo pia itakuwa chuo kikuu kamili.
Alisema chuo hicho kinatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi wa kwanza ifikapo Oktoba, mwakani. “Mwaka ujao wa masomo utakaoanza Oktoba, 2026 Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – Kampasi ya Lindi kitapokea wanafunzi wa kwanza; vivyo hivyo kwa kampasi za Bukoba na kule Zanzibar,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Mkuu mstaafu, Kassim Majaliwa kwa kusaidia upatikanaji wa ardhi wilayani Ruangwa ambako Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimejenga tayari kituo cha utafiti wa kilimo.
Naye, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anayesimamia Fedha, Utawala na Mipango, Prof. Bernadeta Killian alisema ujenzi wa chuo hicho unafuata masterplan ya miaka 20 (2025-2045) kutegemea na uwezo wa Serikali na uwepo wa bajeti. “Mradi wote utagharimu sh. bilioni 14.8 na kati ya hizo, sh. bilioni 13.7 ni za mkandarasi ambaye tayari amelipwa sh. bilioni 5.9. Shilingi bilioni moja ni za kumlipa mshauri mwelekezi.”
Akitoa maelezo ya ujenzi huo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Killian ambaye pia ni msimamizi wa mradi wa kuendeleza elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) alisema majengo mengi yanaendelea yakiwemo ya utawala, vyumba vya mikutano, madarasa sita yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 60 kila moja, karakana ya mafunzo na maabara yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 125 kwa wakati mmoja.
Alisema kampasi hiyo pia ina mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 200 lakini kuna nafasi ya kuongeza ghorofa tatu kila moja na hivyo kuweza kuchukua wanafunzi 800.
