Featured Kitaifa

DC ARUSHA AIPONGEZA TARURA KWA UBUNIFU WA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA

Written by Alex Sonna

Arusha

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude ameipongeza Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa ubunifu katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kutumia teknolojia ya mawe.

Hayo ameyasema leo tarehe 17 Desemba, 2025 alipotembelea Banda la Wakala akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi katika kufunga mkutano wa 18 wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi unaofanyika jijini Arusha.

“Upungufu wa bajeti usiwe ni wimbo bali tuongeze ubunifu, nawapongeza sana TARURA kwa kujenga barabara na madaraja ya mawe. Nadhani teknolojia hii tuiindeleze hasa maeneo ya vijijini kwa barabara ambazo tunazihudumia kwani tutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa”, amebainisha Mhe. Mkude.

Naye, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu TARURA, Mhandisi Edward Amboka amemueleza Mkuu wa Wilaya kuwa TARURA inahudumia mtandao wa barabara nchini zenye urefu wa Kilomita 144,429.77.

Ameeleza kuwa ukubwa huo wa Mtandao wa barabara zinazohudumiwa na TARURA ndio unaopelekea kuonekana kuna upungufu wa bajeti ndio maana wamekuwa wakibuni namna mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo kwa kutumia teknolojia mbalimbali kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchini.

Mkutano wa Tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi ulianza Desemba 15, 2025 na kuhitimishwa leo Desemba 17, 2025 jijini Arusha ukibeba kauli mbiu inayosema “Mifumo Jumuishi ya Usafirishaji ni Msingi Muhimu wa Ukuaji wa Uchumi kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Tanzania 2025”.

About the author

Alex Sonna