Waziri wa maji Jumaa Aweso akizungumza kwenye kongamano hilo jijini Arusha leo.
….
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika kuleta mapinduzi ya huduma za majisafi na usafi wa mazingira barani Afrika wakati akifungua rasmi Kongamano la Maji na Maonesho ya Mwaka 2025 (AWAC 2025) lililofanyika katika Ukumbi wa Corridor Spring jijini Arusha.
Waziri Aweso amesema upo umuhimu kwa Wizara ya Maji na Sekta Binafsi kuwa karibu zaidi ili kufikia malengo ya Serikali na kuipeleka Sekta ya Maji katika hatua nyingine. “Ni wakati muafaka kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi ili tuweze kuendeleza mapinduzi makubwa katika Sekta ya Maji”, Mhe. Aweso amesisitiza.
“Natamani kuona Sekta Binafsi ambao ni moyo wa maendeleo ya Sekta ya Maji, ikiwekeza zaidi kwenye kupunguza changamoto ya upotevu wa maji, ununuzi wa dira za maji, kujenga uwezo kwa wataalam wa Sekta ya Maji, kuimarisha matumizi ya teknolojia, kuongeza vyanzo vya mapato na maeneo mengine.
Waziri Aweso amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Maji na kuitaka Sekta Binafsi kuongeza mchango wake ili nchi iweze kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan SDG 6 inayohusu huduma ya majisafi na usafi wa mazingira.
Aweso amesema ongezeko la idadi ya watu, ukosefu wa miundombinu na mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kwa rasimali maji kwani inahitajika nguvu ya pamoja kupata suluhu.
Ametoa wito kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya Sekta Binafsi na Umma ili kupata suluhu endelevu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri, amewahimiza wadau kuyatumia maudhui ya kaulimbiu ya mwaka huu kama sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maji (Toleo la 2025) ambayo inaeleza wazi umuhimu wa Sekta Binafsi katika ujenzi na uendeshaji wa miradi ya maji.
Ameweka msisitizo katika mkakati wa kusimamia, kulinda na kutunza vyanzo vya maji pamoja na ujenzi wa mabwawa makubwa kwa lengo la kuhakikisha usalama wa maji nchini.
Kongamano hilo lililoandaliwa na Jumuiya Watoa Huduma za Maji Tanzania (ATAWAS) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji limeambatana na maonesho ya huduma na bidhaa mbalimbali za mamlaka za maji nchini, kampuni na taasisi za ndani na nje ya nchi.
Aidha, kongamano limehudhuriwa na washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo wataalamu wa Sekta ya Maji, watafiti, wawekezaji na taasisi za kimataifa. Kaulimbiu yake ikiwa “Kuendeleza Mapinduzi ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira Afrika Kupitia Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi”.
Kongamano hilo la siku tatu linajumuisha mawasilisho ya wataalamu, mijadala ya kitaalam, maonyesho ya teknolojia bunifu, pamoja na fursa za uwekezaji katika Sekta ya Maji.


