
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa tatu kushoto), akiwa katika picha na wajumbe wengine walioshuhudia tukio la uwasilishaji wa Ripoti ya Mapato kwa nchi za Afrika na kushiriki mjadala katika Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi-Afrika-OECD, liliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Paris, nchini Ufaransa)
Na Benny Mwaipaja, Paris, Ufaransa
Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesisitiza kuwa Tanzania imejikita katika kutumia mapato ya ndani kama kipaumbele cha kwanza katika kugharamia miradi ya maendeleo na mageuzi ya kiuchumi.
Mheshimiwa Balozi Omar, amesema hayo wakati akiwasilisha ramani ya kiuchumi ya Tanzania katika Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi-Afrika-OECD, liliofanyika jijini Paris nchini Ufaransa, akiwa miongoni mwa wanajopo 7 walioalikwa rasmi kuwa wazungumzaji katika Jukwaa hilo.
Akipokea pongezi za waandaaji wa Jukwaa hilo, Shirika la Kimataifa la Ushirikino wa Kiuchumi na Maendeleo lenye Makao yake Makuu Paris nchini Ufaransa, (Organisation for Economic Co-operation and Development-OECD), kuhusu hatua kubwa ambazo Tanzania imepiga katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii, Mhe. Balozi Omar alieleza kuwa hatua zilizopigwa ni malengo ya nchi kujitegemea.
Alisema kuwa kwa mwaka wa fedha wa 2026/27, Tanzania inalenga kufadhili asilimia 75 ya bajeti yake kupitia rasilimali zake za ndani, huku asilimia 25 iliyobaki ikitokana na mikopo inayolenga kuziba pengo hilo la kibajeti.
“Mikakati mikuu ya kufikia hili ni pamoja na kulinda wigo wa kodi, kupunguza matumizi, kudhibiti ukwepaji, na kuboresha usimamizi wa kodi” alisema Mhe. Balozi Omar.
Alisema kuwa pamoja na mafanikio hayo, Tanzania bado iko katika hatua ya uwekezaji, ikihitaji rasilimali nyingi kwa ajili ya miundombinu, kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, na nishati, pamoja na maendeleo ya rasilimali watu.
Mhe. Balozi Omar alisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kimuundo, hasa kupitia viwanda, vikiwemo viwanda vya sekta ya kilimo, na uongezaji thamani wa madini, ili kuhakikisha Tanzania inaondokana na njia za jadi za vyanzo vya mapato, huku akipigia chapuo kundi kubwa la vijana wanaohitaji ajira.
Aidha, Mhe. Balozi Omar, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na taasisi za kimataifa kama OECD pamoja na wawekezaji binafsi, ili kuwezesha upatikanaji fedha kwa njia nafuu na inayotabirika.
Akizungumzia umuhimu wa Tanzania kushiriki mikutano na majukwaa hayo ya kimataifa, Mhe. Balozi Omar alisema ni njia muhimu ya nchi kuwasilisha agenda zake za kimkakati za kukuza uchumi wa nchi pamoja na kubadilishana uzoefu na wadau wengine wakiwemo washirika wa maendeleo namna ya kutatua changamoto zinazozikabili nchi nyingi duniani zikiwemo za Afrika na kutafuta mbinu za pamoja za kuzitatua.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla, na Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade.



