Featured • Kitaifa

SERIKALI KUTUMIA MWONGOZO WA BAJETI YA MWAKA 2027/28

Written by Alex Sonna

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb), akiwasilisha kwa Niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati (2026/27 – 2028/29), bungeni jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akifuatilia Bunge la 13, Mkutano wa Tano (5), kikao cha Pili (2), ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb), amewasilisha kwa Niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali Katika Muda wa Kati (2026/27 – 2028/29), bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF – Dodoma)

Na. Asia Singano, WF -Dodoma

Serikali imependekeza kuendelea kutumia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali wa Muda wa Kati wa mwaka 2026/27 hadi 2028/29 katika kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2027/28, huku ikipanga kufanya mapitio ya maeneo muhimu ili kuhuisha taarifa na vipaumbele vya bajeti hiyo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb), wakati akiwasilisha Bungeni Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika Muda wa Kati (2026/27 – 2028/29), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb).

Alisema kuwa Serikali imeona ni vyema kuendelea kutumia Mwongozo uliopo badala ya kuandaa mwingine unaojitegemea.

“Kwa kuwa Serikali iliandaa Mwongozo wa Muda wa Kati unaoanzia mwaka 2026/27 hadi 2028/29 ambapo mwaka 2027/28 umejumuishwa katika kipindi hicho, Serikali inapendekeza Mwongozo huo uendelee kutumika katika maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2027/28 badala ya kuandaa mwongozo mwingine unaojitegemea” alisema Mhe. Profesa Mkumbo.

Alifafanua kuwa pamoja na kuendelea kutumia Mwongozo huo, Serikali itafanya mapitio ya taarifa mbalimbali ili kuhakikisha unaendana na mahitaji ya maandalizi ya bajeti ya mwaka husika.

Alieleza kuwa maeneo yatakayopitiwa ni pamoja na hali ya uchumi jumla, utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/27, vipaumbele vya kibajeti na makadirio ya mfumo wa bajeti kwa kipindi cha mwaka 2027/28 hadi 2029/30 ambapo mapitio hayo pia yatahusisha utekelezaji wa maelekezo ya kimkakati yaliyomo kwenye mwongozo.

Katika hatua nyingine, Serikali inatarajia kupitia muundo wa gharama za uendeshaji wa shughuli za Serikali, usimamizi wa mikataba ya umma na ushiriki wa wazawa katika zabuni, maeneo yanayolenga kuboresha matumizi ya fedha za umma na utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Matokeo ya mapitio haya yanatarajiwa kuboresha maandalizi ya vipaumbele vya bajeti ya Serikali na utekelezaji wake ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za umma” alisema Mhe. Profesa Mkumbo.

Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha mapitio hayo, Serikali inapendekeza kuwasilisha Bungeni maboresho ya mwongozo pamoja na mapendekezo ya ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2027/28 mwezi Februari 2027.

Alisema hatua hiyo, itazingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Bajeti, Sura ya 439, na Kanuni za Kudumu za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za mwaka 2025.

Mhe. Prof. Mkumbo alieleza kuwa utaratibu huo pia utasaidia kuimarisha Mfumo wa Mipango na Matumizi ya Fedha za Serikali kwa Muda wa Kati (Medium Term Expenditure Framework — MTEF) na kuwezesha maboresho ya mfumo wa maandalizi ya bajeti unaozingatia programu (Programme Based Budgeting — PBB).

Vilevile, alisema utaratibu huo utaipa Serikali nafasi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na wadau wa bajeti kupitia vikao vya usikilizaji wa maoni (Public Hearings), kwa lengo la kuboresha mchakato wa maandalizi ya bajeti ya Serikali.

Hata hivyo alisisitiza kuwa Serikali itahakikisha Mwongozo unafanyiwa mapitio ili kuhuisha taarifa na shabaha za uchumi jumla, ukomo wa bajeti wa muda wa kati, vipaumbele vya bajeti na tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2026/27.

About the author

Alex Sonna