Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Oktoba 27, 2026, ameelekea Moscow, nchini Urusi, kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa tatu wa Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi utakaofanyika Oktoba 28–29, 2026.
Mkutano huo utakaowakutanisha viongozi wa Urusi na nchi za Afrika na utaongozwa kwa pamoja na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye.
Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Urusi katika masuala ya biashara, uwekezaji, sayansi na teknolojia, nishati, usalama wa chakula, mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya Akili Unde (AI).
Aidha, mkutano huo unatarajiwa kupitisha tamko la pamoja, Mpango Kazi wa Ushirikiano wa Afrika na Urusi kwa mwaka 2027–2029, pamoja na tamko la ushirikiano kuhusu matumizi ya Akili Unde katika shughuli za kiraia.
Aidha, Matokeo yanayotarajiwa katika Mkutano huo ni pamoja na kupitishwa kwa Tamko la Pamoja, kuandaliwa kwa Mpango Kazi mpya wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Urusi na Afrika kwa kipindi cha mwaka 2027–2029, pamoja na kusainiwa kwa nyaraka mbalimbali za kiserikali na mikataba ya kibiashara.
