Featured • Kitaifa

WRRB, WAENDESHA GHALA WAKAA MEZANI KUELEKEA MSIMU WA KOROSHO 2026/27

Written by Alex Sonna

 

Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imefanya mazungumzo na Umoja wa Waendesha Ghala kujadili mazingira ya kiutendaji ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika kuelekea Msimu wa Korosho 2026/27 unaotarajiwa kuzinduliwa Oktoba 12, 2026.

Kikao hicho kimefanyika leo Septemba 29, 2026 jijini Dodoma kimeongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Bw. Asangye Bangu na kuhudhuriwa na viongozi wa Umoja huo pamoja na Watalaamu wa Bodi hiyo, ili kutafuta ufumbuzi wa hoja mbalimbali walizoziibua hivi karibuni.

Miongoni mwa mambo waliyokubaliana katika kikao hicho ni kuzingatia matakwa ya mwongozo wa msimu wa korosho 2026/27 na kwamba masuala yaliyoibuka kinyume na matakwa hayo hayatumika.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw.Bangu amesisitiza ghala zitakazokidhi vigezo stahiki ndio zitapewa leseni katika msimu huo ili kuhakikisha korosho ghafi inahifadhiwa kwenye ghala bora hasa ikizingatiwa kuwapo na tahadhari ya mvua za El nino.

“Maghala yasiyo na viwango yatakataliwa hii ni kutokana tahadhari za mvua za El nino tunataka korosho yetu isiathiriwe na ubora, tunawahimiza wakulima wahakikishe korosho inakaushwa vizuri kulingana na vigezo vya unyevu vilivyowekwa,”amesema.

Naye, Mwenyekiti wa Umoja huo, Bw. Abdulkarim Masoud ameishukuru WRRB kwa kukutana nao na kujadili malalamiko yao ambayo yatawezesha kupata ufumbuzi na kuendelea na msimu huo.

“Hatujafanya hivi kuharibia mtu bali ni njia ya kutafuta ufumbuzi wa malalamiko yetu ili msimu wa korosho ufanyike kwa ufanisi,”amesema.

About the author

Alex Sonna