Featured • Kitaifa

UTEKELEZAJI USIO SAWA WA KANUNI ZA USAFIRI MTANDAO WAZUA WASIWASI WA USALAMA NA USHINDANI

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu

Uchunguzi uliofanywa katika sekta ya usafiri wa mtandao nchini Tanzania umeibua wasiwasi kwamba kutokuwapo kwa usawa katika utekelezaji wa masharti ya udhibiti kunahatarisha usalama wa abiria, huku kukiziweka katika mazingira magumu kampuni zinazowekeza fedha nyingi kutimiza matakwa ya kisheria.

Waandishi wa habari waliojaribu taratibu za usajili walibaini kuwa baadhi ya makampuni yaliwaruhusu madereva wanaotaka kujiunga kuendelea na mchakato bila kuwasilisha kikamilifu nyaraka muhimu, ikiwemo picha, leseni sahihi ya udereva, kadi ya usajili wa chombo, leseni ya LATRA na nyaraka za bima.

Majaribio ya usajili yaliyofanywa kwa kificho yalibaini tofauti kubwa katika masharti ya kuwapokea na kuwahakiki madereva kati ya kampuni moja na jingine. Hali hiyo imeongeza wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wadau kwamba waendeshaji wanaokabiliwa na uangalizi mdogo wa udhibiti wanalegeza masharti ya uhakiki ili kuongeza idadi ya madereva kwa kasi.

Mbinu hiyo inaweza kuharakisha uongezekaji wa madereva kwenye aplikesheni, lakini pia inatengeneza mazingira yasiyo sawa kibiashara. Kampuni zinazolipia leseni, uhakiki wa madereva, bima, mifumo ya uzingatiaji wa kanuni na kodi hubeba gharama ambazo washindani wasiotimiza masharti kikamilifu huziepuka.

Matokeo yake ni kuwapo kwa faida isiyo ya haki katika gharama za uendeshaji, hali inayoweza kuvuruga ushindani wa nauli na kukatisha tamaa uwekezaji wa muda mrefu katika sekta hiyo.

Athari zake kwa usalama nazo ni kubwa. Baadhi ya abiria waliohojiwa walisema wamekutana na akaunti zisizo na picha za madereva, majina yanayoonekana kuwa ya utani badala ya utambulisho unaoweza kuthibitishwa, pamoja na magari yanayofika yakiwa na taarifa tofauti na zile zilizooneshwa kwenye programu.

Kanuni za LATRA zinataka magari ya kukodi kuwa na leseni halali, huku waendeshaji wa makampuni ya taxi mtandao wakitakiwa kuhakikisha madereva na magari yanayosajiliwa yanakidhi viwango vilivyowekwa.

Matokeo ya uchunguzi huo yanaimarisha hoja ya kuitaka LATRA kusimamia masharti ya uzingatiaji wa sheria kwa usawa katika makampuni ya taxi mtandao yote. Ushindani wa haki hauwezi kuwepo ikiwa baadhi ya waendeshaji wanabeba gharama kamili za udhibiti huku wengine wakikua kwa kukwepa masharti hayo.

Utekelezaji wenye usawa ni muhimu katika kulinda abiria, kuhifadhi imani ya wawekezaji na kujenga sekta endelevu ya usafiri wa kidijitali nchini Tanzania.

About the author

Alex Sonna