Na WMA – MWANZA
Wakala wa Vipimo (WMA) umetoa wito kwa Maafisa wanaosimamia ununuzi na ugavi katika taasisi za umma na binafsi kuhakikisha vifaa vyote vinavyohusiana na vipimo vinawasilishwa WMA kwa ajili ya uhakiki kabla ya kupelekwa kwa watumiaji.
Akizungumza leo Septemba 2, 2026 katika Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza, Afisa Ugavi wa WMA, Bi. Rehema Komba amesema ni vema taasisi zinapokamilisha ununuzi wa vifaa vya kivipimo, zisivipeleke moja kwa moja kwa watumiaji bila kuhakikiwa, kwani inaweza lkupelekea hasara kwa serikali na wananchi.
“Tunasimamia mchakato wa manunuzi, lakini baada ya vifaa kufika, tuzikumbushe taasisi zetu kupeleka kwanza Wakala wa Vipimo kwa uhakiki. Msiogope kuchelewa kwa siku chache, bali ogopeni hasara ya miaka,” amesema.
Akifafanua, Bi. Rehema ametoa mfano wa Mamlaka na Kampuni za Maji, ambapo amesema maafisa ugavi katika Mamlaka hizo wanapaswa kushauri na kuhakikisha mita zote mpya za maji baada ya kununuliwa zinapita WMA kwa uhakiki kabla ya kufungwa kwa wateja.
“Kama kila afisa ugavi atatoa ushauri huu mara baada ya kukamilisha manunuzi, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kuhakikisha kuna biashara ya haki na ulinzi wa walaji nchini” ameongeza.
Mtaalamu huyo wa Ugavi amesema WMA ina mitambo ya kisasa inayowezesha kutoa huduma ya uhakiki wa haraka hali inayoepusha usumbufu kwa taasisi wakati wa kutoa huduma.
Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yameanza tarehe 28 Agosti na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 6 Septemba, 2026.
