Featured Kitaifa

UWT YAWATAKA WANACHAMA WA CCM KUHESHIMU KATIBA, KANUNI NA TARATIBU

Written by Alex Sonna

N.Mwandishi Wetu- DODOMA

UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) imeunga mkono uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa wa kumfuta uanachama aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama hicho, Dk. Emmanuel Nchimbi huku ukisisitiza uamuzi huo umelenga kuimarisha misingi ya nidhamu, uwajibikaji na usawa ndani ya Chama.

Umesisitiza kuwa uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia katiba, kanuni, taratibu na miongozo ya CCM, baada ya kubainika kwamba Nchimbi alifanya makosa ya kimaadili na kinidhamu yanayokwenda kinyume cha misingi na taratibu za CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 28.2026  jijini Dodoma , Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda, amesema jumuiya hiyo inawapongeza wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia katiba, kanuni na taratibu za CCM.

“Hatua hiyo ni ishara kwamba CCM inaendelea kusimamia nidhamu na uwajibikaji bila kujali nafasi, cheo au hadhi ya mwanachama.

Amesisitiza: “Ndani ya Chama Cha Mapinduzi hakuna mwanachama aliye juu ya Chama, wala hakuna umaarufu unaoweza kuwa mkubwa kuliko Chama. Hakuna anayeweza kukibagaza Chama halafu akanyamaziwa. Hili halikubaliki.”

Kadhalika, UWT imempongeza Deogratius Ndejembi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais Mteule, uteuzi ambao ni heshima kubwa na uthibitisho wa imani iliyopo kwa Ndejembi kuwatumikia Watanzania.

Chatanda amesema UWT inaamini Ndejembi atatumia nafasi hiyo kwa uadilifu, weledi, uzalendo na kujituma katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

Amesema uteuzi huo unaendelea kuonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuimarisha uongozi, kuongeza ufanisi wa serikali na kusukuma mbele ajenda za maendeleo na ustawi wa Watanzania.

Aliwataka wanachama wa CCM, bila kujali cheo, hadhi au nafasi walizonazo, kuendelea kuheshimu katiba, kanuni, taratibu na miongozo ya Chama, akisema nidhamu ndiyo msingi wa kudumisha umoja na mshikamano.

“Ni lazima kwa yeyote ambaye ni mwanachama wa CCM, bila kujali cheo, hadhi, kabila, dini au vyovyote alivyo, aheshimu taratibu za Chama chetu,” amesema Chatanda.

About the author

Alex Sonna