Featured Kitaifa

RC CHALAMILA ATOA WIKI MOJA KWA MABASI MAKUBWA KUREJEA STENDI YA MAGUFULI

Written by Alex Sonna

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali imechukua hatua mpya za kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuelekeza mabasi makubwa ya masafa marefu kutumia Stendi ya Magufuli kama kituo kikuu cha kuanzia na kumalizia safari zao.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambapo amewataka wamiliki na waendeshaji wa kampuni za mabasi kuanza maandalizi ya utekelezaji wa utaratibu huo kabla ya Agosti 17, 2026. Amesema baada ya tarehe hiyo, mabasi ambayo hayana vibali maalum hayatapaswa kuingia katikati ya jiji kwa ajili ya kupakia au kushusha abiria.

Chalamila amesema utaratibu huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuipangilia upya sekta ya usafirishaji jijini Dar es Salaam, hasa katika maeneo ya katikati ya jiji ambayo yamekuwa yakikabiliwa na msongamano mkubwa wa magari. Kwa sasa, kampuni sita pekee zimepewa vibali maalum vya kushusha abiria katika maeneo ya katikati ya jiji.

“Matumizi ya Stendi ya Magufuli yatasaidia kupunguza idadi ya mabasi makubwa yanayoingia katikati ya jiji, huku abiria watakapofika stendi hiyo wakiendelea na safari zao kwa kutumia usafiri wa ndani, ikiwemo mabasi ya mwendokasi, daladala, bajaji na pikipiki.”amesema RC Chalamila

Aidha, amesema kampuni za mabasi zinaruhusiwa kuandaa huduma za shuttle zitakazosaidia kuwaunganisha abiria kutoka Stendi ya Magufuli na maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam. Hatua hiyo, amesema, inalenga kuhakikisha mabadiliko hayo hayaathiri urahisi wa abiria kufika wanakokwenda.

Chalamila pia amesisitiza kuwa mfumo huo mpya una fursa ya kuchochea shughuli za kiuchumi na kulinda ajira za waendeshaji wa usafiri wa ndani. Amesema mabasi makubwa yanapofanya safari hadi katikati ya jiji na kuwashusha abiria katika maeneo mbalimbali, yanaingilia sehemu ya shughuli ambazo zinaweza kufanywa na watoa huduma wa usafiri wa ndani.

Ameeleza kuwa mfumo unaopangwa utaweka mgawanyo wa majukumu, ambapo mabasi ya masafa marefu yatahusika zaidi na usafirishaji wa abiria kutoka mikoa mbalimbali hadi Stendi ya Magufuli, huku usafiri wa ndani ukiwaunganisha abiria hao na maeneo wanayokwenda ndani ya jiji.

Pia  amewataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi kutumia muda uliotolewa kufanya maandalizi, ikiwemo kuweka mifumo ya kuwasaidia abiria wao wanapofika Stendi ya Magufuli. Amesisitiza kuwa utekelezaji rasmi utaanza baada ya Agosti 17, 2026 na kampuni zisizo na vibali maalum zinatakiwa kuzingatia utaratibu huo.

Hatua hiyo inatarajiwa kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wa mabasi ya masafa marefu jijini Dar es Salaam, huku Serikali ikilenga kupunguza msongamano, kuimarisha usafiri wa abiria na kuongeza ufanisi katika matumizi ya miundombinu ya usafirishaji.

About the author

Alex Sonna