Featured Kitaifa

WANAFUNZI WA MTEMI MAZENGO WATOA ELIMU YA VIPIMO KWA NAIBU WAZIRI LONDO NANE NANE

Written by Alex Sonna

 

Na WMA – DODOMA.

Wanafunzi wa Klabu ya Vipimo (Vipimo Club) kutoka Shule ya Msingi Mtemi Mazengo ya jijini Dodoma, wamegeuka walimu kwa siku moja baada ya kumpa elimu ya vipimo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, katika banda la Wakala wa Vipimo (WMA), kwenye Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane, Dodoma.

Leo Agosti 7, 2026, Naibu Waziri Londo alishangazwa na ufasaha wa wanafunzi hao walipomweleza umuhimu wa vipimo sahihi, kuandika kwa usahihi vifungashio katika bidhaa zilizofungashwa pamoja na madhara ya lumbesa.

“Nimefurahishwa sana. Watoto hawa ni mabalozi wazuri wa jamii. Uwekezaji wa WMA katika kizazi kijacho unaleta matokeo,” alisema.

Wanafunzi hao walikuwa katika ziara iliyoratibiwa na Wakala wa Vipimo ikiwa ni sehemu ya mpango wa elimu ya vipimo kwa vitendo.

 Mkakati wa WMA ni kuwajengea wanafunzi uelewa wa vipimo kwa nadharia na vitendo ambapo leo wanafunzi hao wa Klabu ya Vipimo ndiyo walikuwa wakitoa huduma zote bandani ikiwemo kuelimisha, kuonyesha matumizi ya vipimo mbalimbali na kujibu maswali ya wananchi.

Naibu Waziri Londo ameonesha kufurahishwa na namna wanafunzi hao walivyojengewa uelewa mpana katika masuala ya vipimo na umahiri wao wa kutoa elimu hiyo kwake na kwa wananchi mbalimbali waliotembelea banda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Wakala wa Vipimo, Francis Olwero amesema WMA imejipanga kikamilifu kuendeleza klabu za vipimo za wanafunzi ili kuwajengea uelewa wa kivipimo na kurahisisha zaidi usambazaji wa elimu ya vipimo kwa taifa zima wao wakiwa kama mabalozi. 

Amesema wanafunzi hao wamedhihirisha kuwa mbinu hiyo ya kuwaandaa wanafunzi kwa kuwapatia elimu ya vipimo ina tija.

Kiongozi wa Vipimo Club kutoka Mtemi Mazengo, Glory Enock ameishukuru WMA kuanzisha klabu hiyo na kuwapa elimu ya vipimo huku akibainisha kuwa ziara yao NaneNane ililenga pia kusaidia kujenga utamaduni wa “Pima kwa Haki, Pata Faida Halali”

 “Tumefundishwa, sasa tunafundisha wazazi na wafanyabiashara kutumia mizani sahihi,” alisema.

Wananchi waliotembelea banda la WMA waliipongeza na kuitaka iendelee kushirikisha shule nyingine kuanzisha Klabu za Vipimo.

About the author

Alex Sonna