Na Asha Mwakyonde, DODOMA
Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF),umewataka vijana, wajasiriamali, wakulima, wafugaji na wafanyakazi wa taasisi mbalimbali kutumia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kujiajiri, kuanzisha viwanda vidogo, kuongeza thamani ya mazao na kushiriki katika biashara zinazochochea matumizi ya nishati safi.
Akizungumza leo Agosti 5, 2026 katika Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo Nanenane, yanayoendelea jijini Dodoma, Meneja Masoko na Uhamasishaji wa mfuko huo Linda Mshana, amesema taasisi hiyo imejikita katika kutoa elimu ya fedha pamoja na mikopo yenye lengo la kuinua uchumi wa wananchi kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Amesema mbali na kuwakopesha wajasiriamali, mfuko huo pia unatoa fursa kwa vijana wanaotaka kuanzisha biashara mpya, ikiwemo biashara za kahawa, usindikaji wa mazao, pamoja na biashara zinazohusiana na nishati safi kama vile uzalishaji na uuzaji wa majiko banifu.
“Tunawahamasisha vijana kutumia fursa zilizopo. Unaweza kujifunza kutengeneza kahawa au bidhaa nyingine, kupata mkopo na kuanzisha biashara yako. Hii inachangia kuongeza ajira, kukuza kilimo cha kahawa na kuongeza thamani ya mazao ya ndani,” amesema.
Ameongeza kuwa SELF Microfinance Fund inaunga mkono juhudi za matumizi ya nishati safi kwa kufadhili shughuli na biashara zinazochangia utunzaji wa mazingira, huku ikisaidia wananchi kushiriki katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo kuanzia uzalishaji, uchakataji, usafirishaji hadi masoko.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, mfuko huo tayari umefikisha mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa wanufaika mbalimbali nchini, huku zaidi ya wananchi laki sita wakinufaika na huduma hizo, na matarajio ni kuwafikia watu wengi zaidi.
Ameeleza kuwa masharti ya kupata mkopo ni rafiki, ambapo mwombaji anatakiwa kuwa na shughuli ya uzalishaji au biashara iliyodumu kwa angalau mwaka mmoja ili kustahili kupata huduma hiyo.
Mbali na mikopo, SELF Microfinance Fund pia hutoa elimu ya fedha inayowasaidia wananchi kupanga uwekezaji, kukuza mitaji, kutumia mikopo kwa ufanisi na kuepuka madeni yasiyo ya lazima.
Aidha, amebainisha kuwa taasisi hiyo inatoa huduma za bima, ikiwemo bima ya usafirishaji wa mazao na bidhaa, ambayo husaidia kulinda mali za wafanyabiashara endapo kutatokea hasara wakati wa usafirishaji.
SELF Microfinance Fund imewataka wananchi kutembelea banda lao katika Maonesho ya Nanenane ili kupata elimu, ushauri na kufahamu fursa mbalimbali za mikopo na huduma nyingine zinazotolewa kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi.