Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza kuwa mageuzi ya elimu nchini lazima yaendane na mahitaji ya uchumi wa taifa kwa kutoa ujuzi unaohitajika kwa vijana.
Akizungumza Julai 14, 2026 jijini Dodoma katika kikao na Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu na Wakuu wa Vyuo, Prof. Mkenda amesema Vyuo Vikuu ndio vina vijana wengi hivyo kuna kazi kubwa ya kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana hao pamoja na malezi ili waweze kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi nchini na hata nje ya nchi.
Aidha, Prof. Mkenda amebainisha kuwa mageuzi ya elimu yanayotekelezwa kupitia vyuo vikuu lazima yafungamanishwe na Dira 2050 na mipango mkubwa ya nchi na mwelekeo wa kidunia katika uchumi, sayansi na Teknolojia.
Amesisitiza kuwa kampasi mpya zilizojengwa zilenge kutoa ujuzi wa moja kwa moja, ili kuandaa wataalamu wanaohitajika katika uchumi wa nchi badala ya zilezile zilizopo.
Pia amesisitiza kuwa miaka kumi ya elimu ya lazima iwe na mikakati thabiti ya utekelezaji, na kipaumbele kikuu kiwe elimu ya ujuzi.
Amevitaka vyuo vikuu kuanzisha mafunzo ya walimu wa amali na ufundi ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Prof. Mkenda amesisitiza kuwa Dira itatekelezwa na vijana wenye ujuzi, hivyo sekta ya elimu inapaswa kuendelea kuwekeza nguvu katika elimu ya ufundi na mafunzo ya amali.
