Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Asha Juma Ferouz, akiwasilisha Mpango wa Bajeti wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 7,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeshauri mambo saba kwa Serikali ikiwemo kuhakikisha fedha za miradi na shughuli za elimu zinatolewa kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Akiwasilisha maoni hayo kwa niaba ya kamati,bungeni Mjumbe wa Kamati hiyo Asha Juma Ferouz amesema Kamati imeishauri Serikali kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu, ikiwemo kuhakikisha fedha za miradi na shughuli za elimu zinatolewa kwa wakati ili kuharakisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
Pia ushauri mwingine ni kuongeza fedha kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa Vyuo vya VETA 64 vya Wilaya pamoja na chuo kimoja cha Mkoa wa Songwe.
Vilevile,kuhakikisha fedha za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu zinatolewa kwa ukamilifu na kwa wakati ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi kunufaika.
Pia,kuanzisha au kuimarisha hospitali za mafunzo kwa vyuo vikuu vinavyotoa elimu ya afya,kuboresha upatikanaji na usambazaji wa vitabu ili kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.
Mjumbe huyo aliutaja ushauri mwingine ni Kuboresha mfumo wa utoaji wa ruzuku ya uthibiti ubora kwa kuhamisha fedha hizo kwenda Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia badala ya TAMISEMI
Vilevile,Kuongeza bajeti ya mafunzo kazini kwa walimu, hususan walimu wa lugha ya alama na elimu jumuishi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Mjumbe huyo alisema kamati imeeleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo utasaidia kuboresha ubora wa elimu, kuongeza ufanisi wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha rasilimali watu inaimarishwa kwa ajili ya uchumi wa kisasa.