Na.Alex Sonna,Mzalendo blog-DODOMA
Serikali imeeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa ya wanawake kukosa nguvu ya kufanya maamuzi ya kiuchumi, kijamii na kimazingira licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea za kuwawezesha wanawake nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua matokeo ya Tafiti za Uwezeshaji Wanawake na Lishe 2023/24 pamoja na Utafiti wa Jinsia na Mazingira 2025 jijini Dodoma.
Waziri huyo amesema kuwa matokeo ya tafiti hizo yanaonesha kuwa wanawake wengi bado hawajiamini kushiriki katika maamuzi muhimu yanayohusu fedha, mali, ndoa, uzazi na hata matumizi ya rasilimali za mazingira.
Amesema ni asilimia 26 pekee ya wanawake wanaoamini kuwa mwanamke anapaswa kuwa huru kufanya maamuzi kuhusu shughuli zake za kiuchumi, huku asilimia 34.1 tu wakikubali mwanamke kuwa na uhuru wa kufanya maamuzi kuhusu ndoa, talaka na uzazi.
“Takwimu hizi zinaonesha bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kuongeza elimu na uhamasishaji kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia,” amesema Dkt.Gwajima
Aidha, amesema zaidi ya nusu ya wanawake nchini bado hawana ushawishi katika matumizi ya fedha ndani ya familia ambapo wanaume wanaongoza kwa asilimia 54.8 ya maamuzi ya kifedha ikilinganishwa na wanawake wenye asilimia 39.6.
Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wengi hushiriki katika vikundi vya kijamii visivyo rasmi kama vikoba na vikundi vya dini, lakini ni asilimia tisa tu wanaojihisi kusikilizwa katika jamii, tofauti na wanaume ambao ni asilimia 26.
Katika upande wa lishe, Waziri Gwajima amesema utafiti umebaini kuwa mwanamke aliyewezeshwa kiuchumi ana nafasi kubwa ya kuboresha lishe ya familia yake.
“Matokeo yanaonesha wazi kuwa uwezeshaji wa mwanamke una mchango mkubwa katika ustawi wa familia na maendeleo ya taifa,” amesema
Kwa upande wa mazingira, amesema wanawake ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi kutokana na majukumu yao ya kila siku, ikiwemo kutafuta kuni na maji.
“Asilimia 82.9 ya wanawake wameathiriwa na angalau athari moja ya mabadiliko ya tabianchi, huku ukame ukiwa changamoto kubwa zaidi hasa maeneo ya vijijini.”amesema
Waziri huyo ameeleza kuwa karibu asilimia 81 ya kaya za vijijini bado zinategemea kuni kwa ajili ya kupikia, hali inayochangia uharibifu wa mazingira na kuongeza mzigo kwa wanawake.
Pia amesema zaidi ya asilimia 80 ya wananchi wanafahamu athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini bado wanawake wengi hawapati taarifa muhimu za tahadhari za majanga kwa wakati.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha uwezeshaji wa wanawake kupitia elimu, mikopo, umiliki wa mali, ushiriki wa maamuzi na matumizi ya takwimu sahihi katika kupanga maendeleo.
“Kuwawezesha wanawake sio suala la haki pekee, bali ni uwekezaji muhimu katika uchumi, lishe bora na ustahimilivu wa mazingira,” amesisitiza
Tafiti hizo zimefanywa kwa ushirikiano kati ya Serikali, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), wadau wa maendeleo pamoja na mashirika ya kimataifa likiwemo FAO, UN Women na Benki ya Dunia.
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Amina Msengwa, amesema kuwa uzinduzi wa tafiti hizo unakwenda sambamba na utekelezaji wa dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2050, ambayo inalenga kujenga uchumi jumuishi unaozingatia usawa wa kijinsia na kuinua nafasi ya wanawake kiuchumi na kijamii nchini.
Naye Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ,Salum Kassim Ali, amesema tafiti hizo ni muhimu katika kutoa mwelekeo sahihi wa kisera na kiutendaji, akibainisha kuwa zinasaidia kuonesha hali halisi ya ushiriki wa wanawake katika maendeleo na hivyo kuwezesha mipango bora zaidi ya kuwawezesha wanawake nchini.
