Na Mwandishi Wetu, DODOMA
Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimeishauri Serikali kufanya mageuzi ya kina katika mfumo wa kodi ili kuongeza mapato ya ndani bila kuongeza mzigo kwa wafanyakazi.
Pendekezo hilo limo katika andiko maalum la ushauri kuhusu kodi na uchumi lililowasilishwa serikalini, likilenga kuboresha ukusanyaji wa mapato na kukuza uchumi wa taifa kwa njia jumuishi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie, mfumo wa sasa wa kodi bado una changamoto ya wigo mdogo wa walipa kodi, hali inayochangia mapato kuwa chini ya kiwango kinachopendekezwa kimataifa.
Alisema uwiano wa mapato ya kodi dhidi ya Pato la Taifa umeendelea kuwa kati ya asilimia 11 hadi 13, chini ya wastani wa asilimia 16 kwa nchi zinazoendelea.
“Tunashauri kupanua wigo wa kodi kwa kujumuisha sekta zisizo rasmi na uchumi wa kidijitali, badala ya kuongeza viwango vya kodi kwa wafanyakazi,” alisema Dk. Loisulie.
Aidha, chama hicho kimependekeza kuanzishwa kwa kodi ya huduma za kidijitali, kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa katika ukusanyaji wa kodi, pamoja na kupunguza mzigo wa kodi kwa wafanyakazi wa kipato cha chini na cha kati.
THTU pia imebainisha kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo unaweza kuongeza mapato ya serikali kwa asilimia 3 hadi 5 ya Pato la Taifa ndani ya kipindi cha miaka mitano, bila kuwaongezea wananchi mzigo wa ziada.
Kwa mujibu wa chama hicho, njia sahihi ya kuongeza mapato si kuongeza kodi, bali ni kupanua msingi wa kodi na kuboresha usimamizi wake.