Na Atley Kuni, WAF – Morogoro
Mkuu wa Huduma za Radiografia kutoka Wizara ya Afya, ndugu Gerald Mrema, amewataka wataalamu wa radiografia kutumia weledi na maarifa yao kuandaa mwongozo utakaotumika kusimamia utekelezaji wa huduma za radiografia kote nchini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mrema ametoa kauli hiyo Machi 17, 2026 mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha siku tatu cha kuangalia na kuboresha mwongozo wa ubora wa huduma za mionzi nchini Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha wataalamu 23 wa huduma za uchunguzi kwa kutumia mionzi (radiolojia), tiba kwa matundu madogo (interventional radiology) pamoja na tiba ya mionzi (radiotherapy), amesema huu ni wakati muafaka wa kupitia na kuboresha miongozo iliyopo ili kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma hizo.
Amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuandaa mwongozo imara unaozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa, akibainisha kuwa matumizi ya mionzi katika uchunguzi na matibabu yameongezeka nchini, hasa katika hospitali za rufaa.
“Lazima tuhakikishe usalama wa wagonjwa na wataalamu unazingatiwa kikamilifu ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya teknolojia ya mionzi,” amesema Mrema.
Kwa upande wake, Dkt. Florah Lwakatare, mwakilishi wa Baraza la Mionzi kutoka Wizara ya Afya, amesema Baraza lina jukumu la kusimamia taaluma na wataalamu wanaotoa huduma za mionzi, ikiwemo kutoa leseni, kukagua vifaa na kuhakikisha kanuni za kinga dhidi ya mionzi zinazingatiwa.
Ameongeza kuwa juhudi hizo zinaendana na azma ya Serikali ya kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora na usalama katika sekta ya afya.
Naye Cecilia Nyabakari, Mratibu wa Huduma za Uchunguzi wa Mionzi kutoka Wizara ya Afya, amesema kuwa maandalizi ya mwongozo huo yanalenga kuleta ufanisi na usawa katika utoaji wa huduma za mionzi nchini.
Amefafanua kuwa mwongozo huo utaweka viwango vya matumizi sahihi ya vifaa tiba kama vile X-ray, CT-Scan, PET-Scan, MRI na mashine za tiba ya mionzi, pamoja na kuboresha taratibu za ulinzi kwa wagonjwa na wahudumu wa afya.
Huduma za mionzi nchini Tanzania zimeendelea kuimarika katika miaka ya karibuni kufuatia uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya afya, ikiwemo uboreshaji wa hospitali za rufaa za kanda na taifa pamoja na kuongezeka kwa wataalamu waliobobea katika fani hiyo. Hata hivyo, bado kuna haja ya kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma hizo katika maeneo ya pembezoni.
Kukamilika kwa zoezi hilo, Wizara ya Afya inatarajia kushirikisha wadau mbalimbali katika utekelezaji wa mwongozo huo, wakiwemo viongozi wa mashirika yanayotoa huduma za afya kama CSSC, APHTA na BAKWATA, pamoja na vyuo vya mafunzo ya afya na hospitali binafsi.
Ushirikishwaji huo unalenga kuhakikisha mwongozo unatekelezwa kwa ufanisi, unazingatia viwango vilivyowekwa na unachangia kuboresha ubora wa huduma za mionzi kwa wananchi wote.
