Kaimu Mkurugenzi Mkuu- wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, leo Machi 05, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, leo Machi 05, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, leo Machi 05, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana, leo Machi 05, 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-Dodoma
Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imesema inaendelea kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi kwa kusimamia ushindani wa haki katika biashara pamoja na kulinda maslahi ya watumiaji, hatua inayochangia pia kufungua fursa za ajira na uwekezaji kwa vijana nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo uliopo Mtumba, Dodoma, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026 tume imeendelea kuruhusu miungano mbalimbali ya makampuni katika sekta tofauti za uchumi ili kuongeza uwekezaji, ushindani wa soko na ajira kwa Watanzania.
Uwekezaji sekta ya kilimo wachochea uchumi
Kwa mujibu wa Ngasongwa, FCC iliridhia miungano miwili ya makampuni katika sekta ya kilimo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 20.4. Miungano hiyo inahusisha kampuni ya Africado Limited na AgDevCo Limited pamoja na muungano wa Amboni Sisal Properties Limited na Amboni Spinning Mill Limited.
Amesema uwekezaji huo utaongeza uwezo wa uzalishaji na usindikaji wa mazao ya kilimo kama parachichi na katani huku ukiongeza ajira kwa wakulima wadogo na vijana wanaojihusisha na shughuli za kilimo.
Mawasiliano na Teknolojia Yachochea Huduma za Intaneti
Katika sekta ya mawasiliano, FCC iliridhia ununuzi wa kampuni ya Habari Node Limited na mfuko wa uwekezaji wa Pembani Remgro Infrastructure Fund II. Muungano huo unatarajiwa kuongeza mtaji na kuboresha huduma za intaneti nchini, hususan katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Tanga na Mara.
Bi.Ngasongwa amesema hatua hiyo itasaidia kupanua upatikanaji wa intaneti ya bei nafuu na kuimarisha shughuli za kidijitali zinazowezesha vijana kushiriki katika uchumi wa kidijitali.
Sekta ya Viwanda Yavutia Uwekezaji Mkubwa
Katika sekta ya uzalishaji viwandani, FCC iliridhia miungano saba yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 103.9. Miungano hiyo inahusisha makampuni yanayozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo sabuni, vifaa vya mabomba ya maji, vifungashio na bidhaa za karatasi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uwekezaji huo utasaidia kuongeza uzalishaji wa viwandani, kuleta teknolojia mpya na kuongeza ajira kwa vijana katika mnyororo wa thamani wa viwanda.
Miradi Mikubwa ya Madini na Nishati
Tume pia iliridhia miungano katika sekta ya madini ikiwemo uwekezaji katika miradi ya Liganga na Mchuchuma yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.3. Miradi hiyo inatarajiwa kutoa mamia ya ajira za moja kwa moja na maelfu ya ajira zisizo za moja kwa moja wakati wa ujenzi na uendeshaji.
Katika sekta ya nishati, FCC iliridhia ununuzi wa hisa katika kampuni ya Songas Limited, hatua itakayosaidia kuimarisha uzalishaji wa umeme na biashara ya gesi asilia nchini.
Utalii, Afya na Sekta ya Fedha
Bi.Ngasongwa amesema miungano kadhaa pia imeidhinishwa katika sekta za utalii, afya na fedha. Katika sekta ya utalii, miungano hiyo inalenga kuimarisha huduma za kitalii na kuvutia watalii zaidi kufuatia juhudi za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia kampeni ya Royal Tour.
Katika sekta ya afya, uwekezaji mpya katika hospitali na kampuni za dawa unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za matibabu na dawa salama kwa wananchi.
Mapambano Dhidi ya Bidhaa Bandia
FCC imeendelea kudhibiti uingizaji na usambazaji wa bidhaa bandia nchini ili kulinda biashara halali na watumiaji. Ngasongwa alisema udhibiti huo unasaidia kuimarisha ushindani wa haki katika soko na kuongeza imani ya wawekezaji.
Ulinzi wa Mlaji Waimarishwa
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026, FCC ilishughulikia jumla ya malalamiko 63 ya watumiaji ambapo malalamiko 45 yalipatiwa ufumbuzi huku mengine yakiendelea kufanyiwa kazi.
Aidha, tume imeendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu masuala ya ushindani na ulinzi wa mlaji kupitia semina, warsha na mikutano ya kitaaluma.
Huduma za FCC kwenda kidijitali
FCC kwa kushirikiana na TradeMark Africa inaendelea kutekeleza mradi wa kuhamisha huduma zake katika mfumo wa kidijitali kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 1.56. Mradi huo unatarajiwa kurahisisha huduma, kupunguza muda wa maamuzi na kuongeza uwazi katika shughuli za tume.
Huduma Zasogezwa Karibu na Wananchi
Kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi, FCC imeanzisha ofisi mpya za kanda katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Mbeya pamoja na ofisi zilizopo Dar es Salaam na Makao Makuu Dodoma.
FCC Yachangia Mapato ya Serikali
Bi.Ngasongwa amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 tume imechangia takribani shilingi milioni 612 katika Mfuko Mkuu wa Serikali, hatua inayosaidia juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi, hususan vijana.
FCC imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda ushindani wa haki katika soko na kumlinda mlaji ili kuhakikisha mazingira bora ya biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi nchini.