Na Edward Winchislaus
Serikali imetangaza kuwa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake mwaka 2026 yataelekeza nguvu zaidi katika uwezeshaji wa kiuchumi na utekelezaji wa haki za wanawake na wasichana kama nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 17, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt.Dorothy Gwajima, amesema maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia Machi 1 hadi 8, 2026 katika ngazi zote kuanzia kijiji hadi mkoa.
Kaulimbiu ya mwaka huu inasema, “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050,” ikilenga kuhamasisha jamii kutambua na kutekeleza haki za wanawake kwa vitendo ili kufikia maendeleo endelevu.
“Kila mkoa utaandaa shughuli zake kwa kuzingatia mwongozo wa kitaifa na kutoa taarifa kwa umma kuhusu ratiba ya matukio. Sare rasmi ya maadhimisho itakuwa ni vazi la batiki litakalotengenezwa na wazalishaji wa ndani, hatua inayolenga kuinua uchumi wa wajasiriamali katika mikoa husika.”amesema Dkt.Gwajima
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo yanaendana na maazimio ya kimataifa chini ya United Nations, hususan yaliyoazimiwa katika Mkutano wa Beijing wa mwaka 1995, ulioweka ajenda ya kuimarisha usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake duniani.
Katika kipindi cha maadhimisho, midahalo na makongamano yatafanyika kujadili nafasi ya mwanamke katika Dira ya Taifa ya 2050, pamoja na kutoa elimu kuhusu huduma za msaada wa kisheria, fursa za kiuchumi na ujasiriamali.
Aidha, maonesho ya wajasiriamali, uzinduzi wa miradi ya kijamii na utoaji wa elimu kuhusu masuala ya nishati safi, hedhi salama na upatikanaji wa mikopo nafuu vitakuwa sehemu ya ratiba ya maadhimisho hayo.
“Wanawake watakaobainika kuwa vinara katika kupinga ukatili wa kijinsia na kuchangia maendeleo ya kiuchumi watatunukiwa tuzo maalum, huku jamii ikihimizwa kushiriki kikamilifu katika shughuli zote.”amesema
Kilele cha maadhimisho ya kitaifa yatafanyika mkoani Geita, na Wizara itatoa tathmini ya ushiriki wa kila mkoa ifikapo Machi 30, 2026.
