Viongozi wa Umoja wa Vyombo vya Habari vya Mitandao ya Kijamii Mkoa wa Dodoma (UMIKIDO), wakiongozwa na Mwenyekiti wao Benny Majata, wamefanya ziara ya kujitambulisha katika Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) – Kanda ya Kati, zilizopo jijini Dodoma.
Ziara hiyo imefanyika leo, Februari 9, 2026, ambapo viongozi wa UMIKIDO walifanya mazungumzo na Meneja wa TCRA Kanda ya Kati, Mhandisi Asajile John. Katika mazungumzo hayo, UMIKIDO ilieleza malengo ya kuanzishwa kwa umoja huo pamoja na dira yake ya kukuza taaluma ya uandishi na uendeshaji wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi wa habari.
Kwa upande wake, Meneja wa TCRA Kanda ya Kati ameukaribisha UMIKIDO na kuahidi ushirikiano wa karibu kati ya pande hizo mbili, ikiwemo kuandaa mafunzo kwa wanachama wa umoja huo. Pia amewahimiza wanahabari wa mitandaoni kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria zilizopo, sambamba na kusajili vyombo vyao na kupata leseni rasmi kutoka TCRA.
Aidha, Mhandisi Asajile John amesema TCRA inaendelea kufanya maboresho mbalimbali yanayolenga kupunguza changamoto na malalamiko ya waendeshaji wa vyombo vya habari vya mitandao ya kijamii, pamoja na kuboresha mazingira ya kazi katika sekta hiyo.
Vilevile, amewahimiza viongozi na wanachama wa UMIKIDO kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali ili kujiimarisha kitaaluma na kiuchumi.
Viongozi wengine wa UMIKIDO walioshiriki ziara hiyo ni Emmanuel Charles (Katibu wa UMIKIDO), Zena Chitwanga (Mhasibu), Daniel Mkate (Afisa Mahusiano), Alex Sonna (Kiongozi wa Kamati ya Ufuatiliaji), Henry Masanja (Kiongozi wa Kamati ya Nidhamu) pamoja na Ronald Sonyo (Kiongozi wa Kamati ya Fedha na Mipango).
