Featured Kitaifa

SERIKALI YAONGEZA KASI YA UCHUMI WA BULUU, DK. NCHEMBA AIPONGEZA TAFICO

Written by Alex Sonna

UWEKEZAJI mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta ya uvuvi umeanza kuzaa matunda kwa kuiwezesha Tanzania kuingia kikamilifu katika uvuvi wa bahari kuu, hatua inayotarajiwa kuongeza ajira, mapato ya Serikali na kukuza uchumi wa buluu.

Hayo yamesemwa leo Agosti 1,2026 na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alipotembelea banda la Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO),katika Maonesho ya wakulima ‘Nanenane 2026″ yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Dk. Nchemba amelipongeza shirika hilo kwa hatua linazoendelea kuchukua katika kuendeleza sekta ya uvuvi na kusema uwekezaji unaofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan umeweka msingi imara wa matumizi yenye tija ya rasilimali za bahari kwa maendeleo ya Taifa.

Amesema sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta za kimkakati zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, kuongeza mapato na kuchangia ukuaji wa uchumi, huku akieleza kuwa dhamira ya Serikali ya kuikuza sekta hiyo inaonekana kupitia uwekezaji mkubwa uliofanyika katika ujenzi wa bandari ya uvuvi pamoja na upatikanaji wa meli za kisasa za uvuvi wa bahari kuu.

Aidha, ameitaka TAFICO kuendelea kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa majukumu yake ili kufikia malengo ya Serikali ya kuongeza mchango wa sekta ya uvuvi katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAFICO, CPA Shaibu Matessa, amesema mafanikio yanayoonekana katika shirika hilo yametokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali imeendelea kuliwezesha shirika hilo kwa kulipatia meli za kisasa za uvuvi wa bahari kuu na kujenga bandari ya kisasa ya uvuvi, ambayo itakuwa kitovu cha shughuli za uvuvi wa bahari kuu nchini.

Matessa ameeleza kuwa bandari hiyo itawezesha meli kushusha mazao ya uvuvi, kutoa huduma za uhifadhi na usafirishaji wa mazao hayo, pamoja na kuchochea ajira na shughuli nyingine za kiuchumi zinazohusiana na sekta hiyo.

Aidha, ameongeza kuwa uwekezaji huo ni sehemu ya mageuzi yanayolenga kuiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone – EEZ), eneo lenye rasilimali nyingi za uvuvi ambalo kwa muda mrefu halijatumika ipasavyo.

“Kwa sasa, TAFICO inamiliki meli moja ya uvuvi wa bahari kuu, huku maandalizi yakiendelea ya kupata meli nyingine mbili katika kipindi cha karibu kupitia ushirikiano na sekta binafsi na mipango ya Serikali ya kuongeza idadi ya meli hizo.

Matessa amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa TAFICO itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinatumika kwa tija, zinazalisha ajira, zinaongeza mapato ya Serikali na kuvutia uwekezaji zaidi katika uchumi wa buluu.

Maonesho ya Nanenane 2026 yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko, Zalisha kwa Tija Kutekeleza Dira ya 2050.”

About the author

Alex Sonna