Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt Rhimo Nyansaho (Mb), Tarehe 08 Januari, 2026 ameendelea na ziara yake ya kikazi kwa kuzitembelea Kamandi mbili za Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi na Kamandi ya Wanamaji jijini Dar-es-Salaam.
Katika ziara yake ya siku moja kutembelea Kamandi hizo mbili, Waziri wa Ulinzi na JKT alipokelewa na Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi, Meja Jenerali Iddi Nkambi ambaye alimpa Dkt Rhimo Nyansaho taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu wa Kamandi hiyo.
Aidha, akiwa katika ziara yake katika Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Mhe Dkt Rhimo Nyansaho, alipewa taarifa ya majukumu ya kamandi hiyo iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Rear Admiral Seif Hassan, na kutembelea Meli za Kivita na karakana ya meli vita na pia kuongea na Maafisa Wanadhimu wa Kamandi hizo.
