Wizara ya Katiba na Sheria ipo katika kikao kazi cha kuhakiki rasimu ya mpango kazi wa Kitaifa wa Biashara na Haki za Binadamu unaohusisha wadau wa Serikali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, wamejengewa uelewa kuhusu kuheshimu haki za binadamu katika nyanja mbalimbali za biashara.
Akizungumza Mjini Dodoma Januari 05, 2026, wakati akifungua kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Franklin Rwezimula amesema kuwa mpango kazi huu wa Biashara na Haki za Binadamu ni mkakati wa kuhakikisha kwamba maendeleo ya kiuchumi na jamii yanakwenda sambamba na heshima ya utu wa Binadamu.
“Mpango kazi huu unalenga kulinda haki za binadamu katika kila hatua ya shughuli za kibiashara na uwekezaji na hukakikisha wafanyakazi wanapata mazingira salama ya kazi, jamii inalindwa dhidi ya unyanyasaji na mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo” Amesema Dkt. Rwezimula.
Aidha Dkt. Rwezimula amesema Biashara na uwekezaji ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi yetu, kuongeza ajira na kuinua ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Bi. Nkasori Sarakikya amesema kuwa Serikali ina wajibu wa kulinda haki za binadamu kwenye mazingira ya biashara, makazini na katika mazingira yote yanayobeba shughuli za binadamu.
