Featured Kitaifa

HALMASHAURI ZITOE TENDA KWA VIKUNDI VYA MIKOPO YA ASILIMIA 10 ILI KUONGEZA WIGO WA AJIRA – PROF. SHEMDOE

Written by Alex Sonna

Na OWM TAMISEMI – Tanga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amezitaka Halmashauri kuvipa kipaumbele vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu vilivyonufaika na mikopo ya aslimia 10 kwa kuvipatia kazi (tenda) ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi.

Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo hivi karibuni, akiwa jijini Tanga katika Uwanja wa Tangamano, mara baada ya kukagua shughuli za vikundi vya wajasiriamali walionufaika na mikopo ya asilimia 10 mkoani Tanga na kuvikabidhi vikundi hivyo hundi ya mikopo ya asilimia 10 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.761.

“Nimeona kikundi cha vijana kilichokopeshwa na kuanzisha mradi wa kufyatua tofali na kimeweza kuajiri vijana wengine, hivyo nazielekeza Halmshauri zenye miradi ya ujenzi kutoa tenda kwa vikundi vya vijana kama hiki cha uzalishaji wa tofali,” Prof. Shemdoe amesisitiza.

Prof. Shemdoe ameongeza kuwa, amejionea kikundi kingine kilichokopeshwa na kuanzisha kampuni ya usafi na sasa kimepewa kazi na TANROADS na TARURA ya kusafisha barabara za jiji la Tanga, hivyo ameilekeza TARURA kwenye mikoa na halmashauri nyingine kuhakikisha wanavipatia vikundi kama hivi kazi kama hiyo ya usafi ili wajiajiri na kujiongezea kipato.

“Nimeshuhudia kikundi cha vijana kinachojishughulisha na ununuzi na uuzaji wa samaki na kingine kinajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, hivyo natoa wito kwa viongozi na wananchi kuviunga mkono kwa kununua bidhaa zao ili viweze kufanya marejesho na kuendelea kuajiri vijana wenzao,” alisema Prof. Shemdoe.

Kwa upande wake, Menyekiti wa Kikundi cha Chapakazi Youth Group kinachojishughulisha na Uzalishaji wa Tofali Bw. Nasibu Mussa, alimshurukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukiwezesha kikundi chake kupata mkopo wa Shilingi Milioni 45 kutoka Halmashauri, ambao umekiwezesha kikundi chake kuongeza mtaji wa uendeshaji katika uzalishaji na uuzaji wa malighafi za ujenzi.

Mnufaika mwingine wa mikopo ya asilimia 10 Bi. Karen Safari, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuinua uchumi wa vijana kupitia mikopo ya asilimia 10 ambayo imewawezesha kujiari wenyewe na kuajiri vijana wengine.

About the author

Alex Sonna