Featured Kitaifa

KEKI KWA MFALME WA PORI! SIMBA WA SAANANE WATIMIZA MIAKA 10

Written by Alex Sonna

 

Simba wa Keki maalum kwa ajili ya Simba wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane akijiandaa kula keki maalum
Keki maalum kwa ajili ya Simba wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
 
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane imeandika historia mpya katika sekta ya uhifadhi na utalii Tanzania, baada ya kuadhimisha ‘Birth Day Party’ ya Miaka 10 ya Simba inaowahifadhi.
 
Sherehe hiyo iliyobeba kaulimbiu inayosema “Saanane King Turns 10” imefanyika Jumamosi, Desemba 20, 2025 ikilenga kuongeza hamasa na kukuza utalii kwenye hifadhi hiyo iliyopo katika Ziwa Victoria, jijini Mwanza.
 
Sherehe hiyo ya Mfalme wa Pori, imehusisha matukio ya watalii kuwaona mbashara (live) simba wakilishwa keki maalum, pamoja na kupata simulizi kuhusu tabia, maisha na umuhimu wa wanyamapori hao katika uhifadhi na utalii.
 
Aidha, tukio hilo la kipekee, limeandaliwa ili kuenzi umaarufu wa simba ambao licha ya kuwa na sifa za ukali, jasiri na mahiri katika kuwinda, wameendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii na chanzo muhimu cha mapato kwa taifa kupitia sekta ya utalii.
 
Akizungumza katika sherehe hiyo, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza na Msimamizi wa Kitengo cha Utalii Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Cesilia Nkwabi, amesema simba wana umuhimu mkubwa katika uhifadhi na utalii.
Cesilia Nkwabi
 
“Simba ni miongoni mwa wanyamapori watano wakubwa (big five), ni kivutio kikubwa cha utalii na ni sehemu ya wanyama wanao- balance (sawazisha) mwingiliano wa kiikolojia kwenye maeneo yanayohifadhiwa.
 
“Kwa hiyo, kupitia tukio hili la kuadhimisha Birth Day ya Simba wa Kisiwa cha Saanane, tunaendelea kuhimiza uhifadhi wa wanyamapori na mazingira wanayoishi ili waendelee kuwepo vizazi hata vizazi,” amesema Cesilia.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Himasheria na Ulinzi Mkakati, Pellagy Marandu, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane, Tutindaga George, amesema tukio hilo ni la kihistoria kwa hifadhi hiyo na TANAPA kwa ujumla.
Pellagy Marandu
 
“Tunaadhimisha birth day hii ili pia kuendelea kumtangaza simba katika hifadhi hii ya kipekee, tuendelee kumuenzi na kumthamini,” amesema.
 
Watalii wa ndani, wakiwemo wanafunzi wamepata fursa ya kuuliza na kujibu maswali kuhusu uhifadhi wa simba na wanyamapori wengine, ambapo washindi walipewa zawadi kemkem, ikiwemo mabegi yenye picha ya simba na nembo ya Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane.
Mwongoza Wageni wa hifadhi hiyo, Sanura Heri, amewaelimisha watalii hao kuhusu tabia, makazi na umuhimu wa simba katika mfumo wa ikolojia ya maeneo yanayohifadhiwa.
 
Baadhi ya watalii hao, wakiwemo Japhet Boaz na Debora Japhet, waliipongeza Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane kwa ubunifu wa kuandaa tukio hilo la kihistoria, na wakatoa wito wa kuwahimiza Watanzania kutembelea Hifadhi za Taifa ili kujifunza na kufurahia vivutio vya wanyamapori na mazingira.
 
Wanafunzi wa Chuo cha Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi, wakiwemo Naishon Ngarash Mollel, Safiel Elietiniswi Mnzava, Junior Mzamin Magwali na Ester Anjelo George, wamesema tukio hilo limewapa uelewa mpana kuhusu maisha ya simba.
 
Wamesema wengi wao hawakuwa wanajua kuwa simba anayehifadhiwa ndani ya uzio anaweza kuishi hadi miaka 20, tofauti na anayekuwa huru porini.
Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayosimamiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), ikiwa na hadhi ya kipekee kama hifadhi ya kwanza nchini iliyopo katikati ya mji.
 
Hifadhi hii iko umbali wa kusafiri dakika 10 tu kwa usafiri wa boti kutoka katikati ya jiji la Mwanza, jambo linaloifanya kuwa kivutio rahisi kufikika kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.
 
Mbali na simba (Mfalme wa Pori), Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane ina vivutio vingi vya utalii, ikiwa ni pamoja na wanyamapori wengine kama vile swala, pundamilia, nyumbu, pimbi, tumbili, digidigi, fisi maji na mamba.
 
Pia, hifadhi hii ina huduma za boat safari katika Ziwa Victoria, rock hiking, maeneo ya mapumziko (picnic sites), michezo majini, kutazama machweo ya jua na malazi ya kitalii.
ANGALIA PICHA
PICHA NA KADAMA MALUNDE – Malunde 1 blog

About the author

Alex Sonna