Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Tabora umekamikisha ujenzi wa daraja la mawe lenye urefu wa mita 60.3 katika barabara ya Sasu–King’wangoko–Seleli, Wilaya ya Kaliua, kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa TARURA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Lusako Kilembe, amesema ujenzi wa daraja hilo umegharimu shilingi milioni 526.7 za ufadhili wa Benki ya dunia kupitia mradi wa RISE, programu ya uondoaji vikwazo vya miundombinu hususan katika maeneo ya vijijini.
Mhandisi Kilembe amesema daraja hilo linashika nafasi ya pili kwa urefu kati ya madaraja ya mawe nchini, likitanguliwa na daraja la aina hiyo lililopo Wilaya ya Busega, Mkoa wa Simiyu, lenye urefu wa mita 80.
“Ujenzi wa daraja hili umeokoa shilingi bilioni 1.27 endapo tungejenga daraja la kawaida la simenti na nondo tungetumia shilingi bilioni 1.8, daraja hili linaenda kuchochea uchumi wa wananchi”. Amesisitiza.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 95, huku ujenzi ukitekelezwa na kampuni ya M/S Mgalang’ombe Co. Ltd ya mkoani Tabora, na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Aidha, Mhandisi Kilembe amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuhakikisha barabara zinapitika kipindi chote cha mwaka, kupunguza changamoto za usafiri hasa wakati wa mvua, kurahisisha usafirishaji wa mazao, kukuza biashara, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kama afya na elimu.
Ameongeza kuwa mradi huo utaimarisha mawasiliano kati ya Mkoa wa Tabora na Shinyanga, hatua itakayosaidia kuharakisha maendeleo ya wananchi wa maeneo husika.


