Featured Kitaifa

SERIKALI YAIPONGEZA IAA KWA KUKUZA ELIMU YA JUU NA KUANDAA WATAALAM MAHIRI

Written by Alex Sonna

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) akihutubia wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha, ambapo pamoja na mambo mengine aliwapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu wao hadi kufikia hatua ya kuhitimu masomo yao, akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho na Taifa kwa ujumla.

Na. Joseph Mahumi, WF, Arusha

Serikali imekipongeza Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa mchango wake mkubwa katika kukuza elimu ya juu, kuimarisha uchumi wa kidijitali na kuandaa wataalam mahiri wenye ujuzi, maadili na ushindani katika viwango vya kimataifa.

Pongezi hizo zimetolewa jijini Arusha na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb), katika Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika uwanja wa chuo hicho.

Mhe Mhandisi Munde, alisema kuwa IAA, kimeendelea kuwa taasisi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia elimu, utafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia ya kisasa.

Aliongeza kuwa Menejimenti, Baraza la Uongozi, wahadhiri na watumishi wa Chuo hicho wanafanya kazi kubwa ya kuandaa wataalam mahiri katika fani mbalimbali ikiwemo Uhasibu, Fedha, TEHAMA, Benki, Bima, Masoko, Ununuzi na Ugavi pamoja na Usimamizi wa Biashara.

“Nawapongeza kwa kuwa na Mitaala inayotilia mkazo ufundishaji kwa vitendo na ujifunzaji unaomuwezesha mwanafunzi kuwa tayari kwa kazi (job-ready) mara anapohitimu” alisema Mhe. Munde

Alisema kuwa hali hiyo inahakikisha pia wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika moja kwa moja katika soko la ajira kwenye maeneo kama Uhasibu, Fedha, Manunuzi, TEHAMA, Masoko, Ukaguzi wa Hesabu, Mawasiliano ya Umma, Uchumi, Kodi, Benki, Bima, Utalii, Usimamizi wa Biashara na maeneo mengine.

Alisema kuwa Serikali imeweka mkazo mkubwa katika mageuzi ya elimu ya juu kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao umeiwezesha Chuo hicho kuboresha miundombinu, kununua vifaa vya kisasa vya TEHAMA, pamoja na kuwawezesha wahadhiri kupata mafunzo ya mbinu za kisasa za ufundishaji, sambamba na kukuza uchumi wa viwanda na uchumi wa kidijitali, ikiwa ni kuhakikisha elimu ya juu inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi, ubunifu na maadili.

Miongoni mwa hatua zilizotajwa ni uanzishwaji wa madarasa janja (smart classes), maabara za kisasa za TEHAMA, maktaba ya kisasa na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika ufundishaji.

Aidha, aliipongeza IAA kwa kuanza utekelezaji wa azma ya Serikali ya kujenga matawi ya vyuo vya elimu ya juu katika mikoa yote nchini, kupitia ujenzi wa Kampasi ya Songea na kuanzishwa kwa Kampasi mpya ya Bukombe kuanzia mwaka wa masomo 2025/2026.

Alisema kampasi hizo zitachangia sio tu maendeleo ya elimu bali pia kukuza uchumi wa wananchi na maeneo husika.

“Kampasi hizi zitakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” aliongeza.

Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu wao hadi kufikia hatua ya kuhitimu masomo yao, akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa Chuo na Taifa.

“Taifa linahitaji vijana kama ninyi; wabunifu, wachapakazi, wanaojifunza kila siku na wanaoweza kutatua changamoto za jamii,” alisema.

Aliwataka wahitimu kutumia elimu waliyoipata kama nyenzo ya kujijenga kimaisha, kuchochea maendeleo ya familia zao na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa uadilifu na weledi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, aliishukuru Wizara ya Fedha ambayo ni Wizara mama ya Chuo hicho, kwa kukiwezesha IAA kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam na Mahafali hayo ni moja ya ushahidi wa wazi kabisa kwa mchango wao katika utekelezaji wa jukumu la msingi la kutoa mafunzo.

Aliongeza kuwa IAA imeendelea kudumisha na kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji kwa kuzingatia miongozo ya mamlaka husika za elimu ya juu, hatua inayochangia kuboresha ufaulu na ushindani wa wahitimu wake katika soko la ajira.

“Wahadhiri wa Chuo wameendelea kushiriki kikamilifu katika tafiti, machapisho ya kitaaluma na makongamano ya kitaifa na kimataifa, hatua inayoongeza hadhi ya Chuo kitaaluma ambapo katika mwaka wa masomo 2024/2025 jumla ya machapisho 20 ya wahadhiri wetu yamechapishwa katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa” alisema Dkt. Tulli.

Naye Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Eliamani Sedoyeka, alisema kuwa Chuo hicho kimeendelea kupanua wigo wa programu zake za kitaaluma kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya Kwanza hadi Shahada za Uzamili, huku tukihakikisha viwango vya ubora vinazingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa.

Prof. Sedoyeka aliongeza kuwa katika mwaka huu wa masomo chuo kimekuwa na jumla ya kozi themanini na moja (81) kati ya hizo; kozi kumi na tisa (19) ni ngazi ya  astashahada /cheti, kozi ishirini (20) ni za ngazi ya stashahada, kozi ishirini na saba (27) ni ngazi ya shahada na kozi kumi na tano(15) kwa ngazi ya shahada ya uzamili.

“Katika kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Chuo kimeanza utekelezaji wa mpango wa madarasa janja (Smart Class) na kampasi janja (Smart Campus), ambapo mpango huu unalenga kutumia TEHAMA kikamilifu katika ufundishaji, tathmini na usimamizi wa shughuli za Chuo” aliongeza Prof. Sedoyeka.

Katika Mahafali hayo ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha, jumla ya wahitimu 4821, katika ngazi ya astashahada, stashahada na shahada katika fani mbalimbali, ambapo kati ya hao wanaume ni 2810 na wanawake 2011.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) (mwenye joho jekundu), akiongoza Maandamano ya Kitaaluma wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha, ambapo Mhe. Munde, alikuwa Mgeni Rasmi.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) akihutubia wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha, ambapo pamoja na mambo mengine aliwapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu wao hadi kufikia hatua ya kuhitimu masomo yao, akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa Chuo hicho na Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) (Hayupo pichani), wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa chuo hicho, jijini Arusha

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) akiwatunuku wahitimu wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa chuo hicho, jijini Arusha.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, akizungumza wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) (Hayupo pichani), wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, akizungumza wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha.

Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi. Mshamu Ali Munde (Mb) (Katikati aliyeketi mwenye joho jekundu), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wahitimu pamoja na wafanyakazi wa taaluma wa Chuo cha Uhasibu Arusha wakati wa Mahafali ya 27 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), yaliyofanyika katika uwanja wa Chuo hicho, jijini Arusha, ambapo Mhe. Munde, alikuwa Mgeni Rasmi.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Arusha)

About the author

Alex Sonna