Featured Kitaifa

LUSWETULA: VIJANA TUMIENI MITANDAO YA KIJAMII KUBUNI FURSA ZA KUJIKWAMUA KIUCHUMI.

Written by Alex Sonna

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akiwatunuku wahitimu (hawapo pichani) katika Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Na. Ramadhani Kissimba, WF – Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Degratius Luswetula (Mb), amerejea wito wake kwa vijana kutumia teknolojia hususani Akili Mnemba (AI) na mitandao ya kijamii ili kubuni fursa za kiuchumi na kuongeza kipato.

Mhe. Luswetula amesema hayo wakati wa Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) -Kampasi ya Dar es Salaam, Zanzibar na Tanga yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo hicho, Kurasini jijini Dar es Salaam.

Mhe. Luswetula alisema kuwa matumizi ya teknolojia yakitumika vizuri itawajengea vijana kujiamini, kufikiri kwa ubunifu na kuwa wazalishaji wa fursa badala ya kuwa watafuta ajira pekee.

Aidha Mhe. Luswetula aliwaasa vijana kuwa watengeneza maudhui (content creator) wenye tija na wanaozalisha maudhui yenye thamani, yanayongeza kipato, kuzingatia maadili na kufuata sheria na taratibu za nchi.

‘’Katika dunia ya sasa, tumieni teknolojia, hususan Akili Mnemba (AI) na mitandao ya kijamii, kubuni fursa za kiuchumi na kuongeza kipato. Vijana wa leo wanaita hii kuwa ‘content creator’ nawasihi muwe content creator wenye tija, wanaozalisha maudhui yenye thamani, yanayoongeza kipato kwa njia halali, kuzingatia maadili na kufuata sheria na taratibu za nchi yetu’’. Alisisitiza Mhe. Luswetula.

Katika mahafali hayo Mhe. Luswetula aliwataka wahitimu kutumia elimu na maarifa waliyoyapata chuoni kama mtaji wa maisha yao kwa kuwa Serikali inawategemea kuwa vijana wabunifu, waadilifu na watumiaji mahiri wa teknolojia katika kuleta mabadiliko Chanya katika jamii.

Mhe. Luswetula aliipongeza Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa kujumuisha Kampasi tatu za Dar es Salaam, Zanzibar na Tanga katika Mahafali ya 23 ya Taasisi hiyo na kuongeza kuwa mwelekeo wa maendeleo na faida za kijiografia, Dar es Salaam, Zanzibar na Tanga ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayoendelea kukua kwa kasi na kuwa nguzo ya uchumi wa Taifa na hayo yanachangia kutoa fursa nyingi kwa wahitimu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

‘’Dar es Salaam inaendelea kuwa kitovu cha biashara, bandari na huduma za kifedha, Zanzibar ni lango muhimu la utalii, uchumi wa buluu na biashara ya bandari, huku Tanga ikiwa na nafasi ya kimkakati, viwanda na utalii wa fukwe. Maeneo haya yanatoa fursa nyingi kwa wahitimu wetu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa’’ Aliongeza Mhe. Luswetula.

Akiongea kwenye mahafali hayo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Prof. William Pallangyo alisema kuwa Taasisi imeendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika Kampasi za Mtwara, Mbeya, Mwanza na Kigoma, huku shughuli za ujenzi zikiendelea katika Kampasi za Singida, Mwanza na Zanzibar ambapo Jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 59 zimetumika kupitia Mradi wa HEET na mapato ya ndani ya Taasisi katika ujenzi wa Kampasi hizo.

Prof. Pallangyo aliongeza kuwa Taasisi ya Uhasibu Tanzania imeanzisha kozi mpya za shahada ya Uzamili zinazolenga kukuza ujasiriamali, ubunifu na usimamizi wa miradi ili kuwaandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko.

‘’Katika Mwaka wa Masomo 2025/2056 TIA imeanzisha kozi mpya za Shahada ya Uzamili zinazolenga kukuza ujasiriamali, ubunifu na usimamizi wa miradi ya maendeleo. Lengo letu ni kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira, teknolojia na mwelekeo na Mpango wa Maendeleo ya Taifa (2050)’’ Alisema Prof.Pallangyo.

Prof. Pallangyo aliongeza kuwa Katika kuendeleza taaluma na ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi, Taasisi imehimiza mafunzo ya vitendo na ubunifu kupitia mashindano ya Mawazo Bunifu (Business Ideas Competitions) katika kampasi zote nane ambapo kupitia mpango huu umewezesha wanafunzi kushiriki katika ziara za kielemu katika vyuo mbalimbali barani Afrika.

‘’ Kupitia mpango huu, mwaka 2023/24 wanafunzi walishiriki ziara za kielimu katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya (Kenya). Mwaka 2024/25 walipelekwa Chuo Kikuu cha Makerere (Uganda). Mwaka huu maandalizi yanaendelea ya kuwapeleka washindi wa kampasi zote Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini’’ aliongeza Prof. Pallangyo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Laurent Degratius Luswetula (Mb), Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Profesa Jehovaness Aikael alisema bodi inaweka mkazo mkubwa katika ubora wa elimu, maadili, uwajibikaji na uadilifu ikitambua kwamba elimu bora haipimwi kwa maarifa pekee bali kwa uwezo wa Taasisi kulea wahitimu wenye tabia njema, weledi na uwezo wa kuaminika katika jamii na za kazi.

Profesa Aikael alisema kuwa Bodi ya ushauri ya Wizara imeendelea kusimamia muelekeo wa kimkakati wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania kwa lengo la kuifanya TIA kuwa Taasisi shindani kitaifa na kikanda, kwa kuhakikisha mitaala, mbinu za ufundishaji na mazingira ya kujifunzia vinaendana na mahitaji ya sasa na baadae kiuchumi, kwenye soko la ajira na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

‘’Katika kusimamia mwelekeo huo, Bodi ya ushauri ya Wizara inaendelea kusisitiza umuhimu wa kuandaa wahitimu wanaoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ikiwemo matumizi yenye weledi na uwajibikaji ya Akili Bandia (Artificial Intelligence) ili kuongeza ubora, ufanisi na ushindani wa rasilimali watu’’ alisema Prof. Aikael

Katika mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) imejumuisha wahitimu 6,334 kati yao wanawake ni 3,589 na wanaume 2,745 ambao wametunikiwa vyeti katika ngazi mbalimbali kuanzia cheti cha Awali hadi shahada ya Uzamili.


Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (Katikati), akiongoza Maandamano ya Kitaaluma, wakati wa Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akiwatunuku wahitimu (hawapo pichani) katika Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wahitimu wakitunikiwa shahada ya Uzamili na Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Fedha (hayupo pichani) Mhe. Laurent Deogratius Luswetula katika mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na wahitimu waliofanya vizuri zaidi katika mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akiteta jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) wakati wa mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akimpatia zawadi mmoja wapo wa wanafunzi waliofanya vizuri katika Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Profesa Jehovaness Aikael, akizungumza na wahitimu na washiriki wa Mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) yaliyofanyika Katika Viwanja vya TIA, Kurasini Jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha – Dar es Salaam

About the author

Alex Sonna