Featured Kitaifa

MAKAMBA ATAKA WANANCHI KULINDA VYANZO VYA MAJI KWA AJILI YA NISHATI

Written by Alex Sonna

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, leo Novemba 26, 2025, ametembelea na kukagua mradi wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji katika Bwawa la Mtera, linalopakana kati ya mikoa ya Iringa na Dodoma.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi, Mhe. Makamba amesema kuwa wananchi wa mikoa hiyo kwa sasa wanaweza kufurahia umeme wa uhakika.

“Mara baada ya kuboreshwa, mitambo hii inatuhakikishia upatikanaji wa umeme wa kutosha. Kwa ujumla, mikoa ya Dodoma na Iringa itakuwa na umeme wa uhakika,” amesema  Mhe. Makamba

Ameongeza kuwa juhudi hizo za Serikali zisingefanikishwa bila kiongozi mkuu, akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitatua.
Makamba amesema kuwa hadi sasa, zaidi ya shilingi Bilioni 10 zimetumika kurekebisha na kuboresha mitambo miwili ya kuzalisha umeme kwenye Bwawa la Mtera.
Aidha, Mhe. Makamba ametoa wito kwa wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji vya Bwawa la Mtera, ikiwemo Bonde la Ihefu, kulinda vyanzo hivyo kwani nishati ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usambazaji wa Umeme TANESCO, Mhandisi Athanasius Nangali, amesema kituo cha umeme kinafanya kazi vizuri na kuendelea kuzalisha Megawati 80, sawa na hali ya awali.
Amehimiza wananchi kuendelea kuwekeza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kutokana na uhakika wa upatikanaji wa umeme, uliozidi kuimarishwa na kituo kipya cha kupokea na kupoza umeme kilichojengwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

About the author

Alex Sonna