Na.Mwandishi Wetu
WAKALA wa Vipimo (WMA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, umeendesha mafunzo maalum kwa wauzaji wa gesi jijini Dodoma ili kuongeza uelewa kuhusu usalama, uhalali wa biashara na matumizi sahihi ya mizani katika upimaji wa gesi.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa na mawakala, wauzaji wa rejareja, wasambazaji pamoja na wawakilishi wa halmashauri za jiji na wilaya.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma, Said Ibrahim, alisema dhamira ni kuhakikisha bidhaa zinazomfikia mlaji zinakuwa na ujazo sahihi, hususan gesi ya kupikia ambayo matumizi yake yameongezeka kwa kasi nchini.
“Ni muhimu kuhakikisha gesi wanayonunua na kuwauzia wateja imepimwa kwa usahihi, na njia pekee ya kufanya hivyo ni kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo,” alisema Bw.Ibrahim
Aidha, aliwakumbusha wafanyabiashara kuwa kutotumia vipimo sahihi ni kosa kisheria na kunaweza kusababisha hasara kwa mlaji na kwa mfanyabiashara mwenyewe.
Kwa upande wake, Afisa Vipimo wa WMA mkoa huo, Edward Patrick, amehoji ni kwanini wafanyabiashara hao hawaweki mizani katika sehemu inayoonekana na wateja hawawapimii mitungi ya gesi kwasababu wengi wao wanakuwa nayo lakini wanaificha.
“Tatizo ni kwamba mnapima mizani mara moja halafu hamrudii tena. Mizani ya kuuza sukari mnaikagua kila mwaka, lakini ya gesi mnaificha hadi mteja aombe ndipo mnaitoa, wakati tayari imeharibika. Mnapaswa kuwa na mizani na kuitumia,” alisema.
Naye Afisa Udhibiti Ubora kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Husna Kabaju, aliwataka wauzaji wa gesi kuhakikisha wanakuwa na mikataba rasmi na mawakala wanaowasambazia mitungi hiyo.
Baadhi ya wauzaji na wasambazaji waliohudhuria mafunzo hayo walisema yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kutumia mizani iliyohakikiwa, wakiomba mafunzo hayo yaendeshwe mara kwa mara.
WMA imekuwa ikitoa mafunzo hayo katika maeneo mbalimbali nchini ili kulinda haki ya mlaji na kuongeza uaminifu katika biashara zinazohitaji vipimo sahihi, zikiwemo gesi za kupikia. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuboresha mazingira ya biashara ya LPG katika Mkoa wa Dodoma kwa kuongeza ubora wa huduma, kuimarisha usalama na kuendeleza taswira ya sekta hiyo nchini.
