Featured Kitaifa

WAZIRI KAPINGA AAGIZA WELEDI NA USHIRIKIANO KATIKA KUENDELEZA UCHUMI WA VIWANDA

Written by Alex Sonna

 

 

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga , ameziagiza menejimenti na watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na ushirikiano ili kutimiza matarajio ya Watanzania wanaosubiri kuona matokeo ya juhudi za serikali katika kukuza biashara na uchumi wa viwanda.

Ametoa wito huo  alipozungumza na menejimenti ya wizara mara baada ya kuwasili ofisini kwake kufuatia hafla ya kuapishwa iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Mhe. Kapinga amesisitiza umuhimu wa kuongeza bidii na ubunifu katika kuendeleza sekta ya viwanda na biashara, akisema juhudi hizo ni muhimu katika kujenga uchumi shindani wa viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Bw. Patrobas Katambi , ametoa rai kwa menejimenti kufanya kazi kwa ushirikiano, upendo na kuzingatia utu wakati wa kutekeleza malengo ya muda mfupi na mrefu ya wizara, ili kuhakikisha Serikali ya Awamu ya Sita inafikia dhamira yake ya kujenga uchumi wa viwanda.

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hashil Abdallah, pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Suleiman Serera, waliwahakikishia Waziri na Naibu Waziri kuwa menejimenti ipo tayari kutoa ushirikiano wote unaohitajika katika kutekeleza jitihada za kuendeleza sekta ya viwanda na biashara kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

About the author

Alex Sonna