Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ametoa wito kwa watumishi wa wizara na taasisi zake kuongeza ubunifu katika kutoa huduma na kuifanya wizara kuwa kimbilio la wananchi.
“Ninatamani kuona ubunifu katika kila Taasisi na Idara. Tumeona matokeo makubwa sana katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria, ambapo wananchi wengi hasa wa maeneo ya vijijini wamekuwa ni wanufaika wakubwa, ninatamani kuona shughuli zenye ubunifu ambazo zitakwenda kuwasaidia wananchi, Tutakesha kuwahudumia watanzania” amesisitiza Waziri Homera.
Dkt. Homera ameyasema hayo leo, 18 Novemba, 2025, katika Ofisi za Wizara, Mtumba jijini Dodoma, akiwa ameambatana na Naibu Waziri Mhe.Zainab Katimba wakati akizungumza na Wakuu wa Taasisi na Menejimenti ya Wizara mara baada ya kuwasili wizarani hapo na kukamilika kwa hafla ya makabidhiano ya Ofisi.
Aidha, Mhe. Waziri amesema matamanio yake ni kuona Wizara inafanya tathmini ya mikoa yenye changamoto kubwa zaidi za Msaada wa Kisheria na kupanga mikakati ya kuifikia mikoa hiyo kwa kuwapeleka wataalamu na kutatua changamoto za Kisheria zilizopo.
Kama sehemu ya kuanza utumishi wake, Waziri Homera amewataka watumishi wa wizara na taasisi zake kufanya kazi kwa bidii na kuongeza ubunifu katika kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Ndg. Eliakim Maswi, amewapongeza viongozi hao wapya kwa kuteuliwa na kuapishwa. Amesema Wizara hiyo imekuwa ni nguzo ya Utawala Bora nchini, hivyo watumishi hawana budi kuiheshimisha historia hiyo kwa matendo.
