Featured Kitaifa

RAIS MWINYI AAGIZA MAWAZIRI KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU NA KUSHUKA HADI KWA WANANCHI

Written by mzalendo

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa agizo kwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao na kushuka hadi ngazi za chini ili kuwahudumia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili badala ya kukaa maofisini.

Akizungumza katika hafla ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri aliowateua hivi karibuni, iliyofanyika leo tarehe 15 Novemba 2025 katika Viwanja vya Ikulu, Mkoa wa Mjini Magharibi, Dkt. Mwinyi amesema Serikali katika Kipindi cha Pili cha Awamu ya Nane itaweka utaratibu maalum wa kutathmini utendaji wa kila wizara pamoja na watendaji wake.

Aidha, Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeanzisha Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa huduma na utekelezaji wa shughuli za Serikali vinafanyika kwa njia ya kidijitali, ikiwemo masuala ya kifedha na ukusanyaji wa mapato.

Pia ameongeza kuwa Serikali imeunda Wizara ya Vijana, Ajira na Uwezeshaji yenye jukumu la kushughulikia changamoto za ajira kwa vijana na kuwawezesha kujiajiri.

Katika mageuzi hayo ya kimuundo, Rais Mwinyi amesema amepunguza idadi ya wizara zilizokuwa chini ya Afisi ya Rais, ambapo sasa zimebaki wizara tatu pekee huku nyingine mbili zikihamishiwa katika maeneo mengine ili kuongeza ufanisi.

Akiwaagiza Mawaziri kuandaa mpango kazi maalum, Rais Mwinyi amesema mpango huo unatakiwa kuzingatia utekelezaji wa ahadi za kampeni, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar, pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Aidha, amesisitiza umuhimu wa Mawaziri kutembelea miradi iliyo chini ya wizara zao ili kufuatilia thamani ya fedha, ubora wa mradi, kiwango cha utekelezaji na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Dkt. Mwinyi amehimiza nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali ikiwemo kupunguza safari za nje, matumizi makubwa ya mafuta, pamoja na kudhibiti udanganyifu na ubadhirifu serikalini. Amewataka viongozi hao kusimamia ipasavyo uwajibikaji wa watendaji walio chini yao, kulinda mali za umma na kupambana na rushwa na uzembe.

About the author

mzalendo