Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), uliyofanyika, Jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya Wataalam, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi pamoja na Kamati za Mawaziri wa Kisekta, ikiwemo Ulinzi, Madini na Jinsia, umebebwa na kauli mbiu ya “Uimarishaji wa Amani na Usalama kwa Maendeleo Endelevu katika Eneo la Maziwa Makuu”
Kupitia kaulimbiu hiyo, nchi wanachama zimejadili hali ya usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu na kupendekeza njia za kuimarisha amani na usalama kwenye eneo hilo.

Katika Mkutano huo, Tanzania inaunga mkono ajenda zote muhimu zilizojadiliwa ikiwemo ya amani na usalama na kusisitiza kuwa itaendelea kutoa mchango mkubwa kama inavyofanya katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa amani ya kweli inapatikana kwenye Kanda hiyo.
Katika Ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mhe. Felix Tshisekedi, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushindi aliyoupata katika uchaguzi huru uliyofanyika mwezi Oktoba 2025.
Aidha, nchi wanachama zimetakiwa kuenzi Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo unaolenga kufikiwa kwa amani, usalama na maendeleo ya kweli kupitia ushirikiano, umoja na mshikamano bila kusahau kujitoa na kujituma kwa hali na mali kufanikisha malengo hayo.
Ajenda zingine zilizojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na masuala ya madini, jinsia pamoja na fedha.
Katika Mkutano huo, Makamu wa Rais ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Zanzibar Mhe. Salehe Juma Mussa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Said Juma Mshana, pamoja na maafisa waandamizi na wataalamu mbalimbali.
