Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imelaani vikali vitendo vya vurugu vilivyotokea nchini Oktoba 29, siku ya uchaguzi mkuu, na kusababisha vifo, uharibifu wa mali pamoja na uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo nchini.
Akizungumza leo Novemba 5,2025 hapa jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu amesema matukio hayo hayapaswi kuungwa mkono kwasababu yanavunja amani katika nchi na kuvunja usalama wa wananchi.
“Sisi kama Tume kutokana na matukio haya tumeamua kufanya uchunguzi wa kina, na tumekwisha jipanga katika jambo hilo ili tuweze kuona ni maeneo yapi ambayo kwa kuangalia matukio yaliyojitokeza tume inaweza kutoa ushauri kwa serikali na vyombo vingine kwa madhumuni ya kutaka kuendelea kulinda amani katika nchi yetu,”amesema.
Amesema katika kipindi kama hicho matukio yaliyojitokeza yamevunja baadhi ya haki za wananchi kwasababu wamepoteza maisha na wengine wamepoteza mali, hivyo wameona ni matukio ambayo wanapaswa kuyafanyia uchunguzi wa kina ili waweze kutoa ushauri kwa namna ya kuweza kuondokana na matatizo ya namna hiyo katika miaka mingine ya uchaguzi.
“Kwa namna yeyote ile matukio yote hayo hayapaswi kuungwa mkono kwasababu yanavunja amani katika nchi na usalama kiujumla,”amesema.
Sambamba na hayo tume imewahimiza wananchi kote nchini kuendelea kutunza tunu ya amani kwa kuzingatia misingi ya katiba na kanuni za nchi kwani inapotokea uvunjifu wa amani kila mmoja anashindwa kufanya shughuli zake za kila siku.