Na Mwandishi Wetu, Kilwa
HIFADHI ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara wilayani Kilwa, Lindi, imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi, baada ya kupokea jumla ya watalii 147 kutoka mataifa 13 duniani waliowasili humo kwa kutumia meli ya kifahari SH Diana tarehe 31 Oktoba 2025.
Watalii hao wametoka katika nchi za Ufaransa, Australia, Ubelgiji, Canada, Uingereza, Uswisi, Ujerumani, Cyprus, New Zealand, Marekani, Urusi, Uturuki na Ukraine. Ziara hiyo iliratibiwa na kampuni za Savannah Tours Ltd kwa kushirikiana na Black Willow Safaris.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya wageni hao, Kamanda wa Hifadhi hiyo, Mhifadhi Mwandamizi Kelvin Stanslaus, amesema ujio wa meli hiyo ni ishara njema kwa ukuaji wa utalii wa urithi nchini, hasa ikizingatiwa umuhimu wa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara kama maeneo yaliyosajiliwa na UNESCO kuwa Urithi wa Dunia tangu mwaka 1981.
“Kupokelewa kwa wageni hawa kunathibitisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa chaguo la kipekee kwa watalii wanaopenda kujifunza historia na kuona urithi wa kiutamaduni,” amesema Mhifadhi Stanslaus.
Aidha, watalii hao walipata fursa ya kutembelea Msikiti Mkongwe na Kasri la Sultani, ambapo walivutiwa na usanifu wa majengo ya mawe pamoja na simulizi za kihistoria kutoka kwa maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) waliobobea katika masuala ya malikale.
Kwa mujibu wa TAWA, ujio wa meli hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuimarisha utalii wa urithi, hususan katika maeneo ya bahari, malikale na visiwa vyenye thamani ya kihistoria.
