Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Augustino Senga, amewahakikishia wananchi Mkoani humo kuwa Mkoa wa Songwe upo salama, wenye utulivu na amani.
Akizungumza Oktoba 24,2025 na askari wa Jeshi la Polisi walioungana na majeshi mengine ya vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani humo baada ya matembezi ya pamoja yaliofanyika Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba Mkoani Songwe, na kuwaeleza maandalizi ya vyombo vya ulinzi na usalama yako vizuri na hakuna sababu ya wananchi kuwa na wasiwasi kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Aidha, Kamanda Senga alieleza kuwa tukio la uchaguzi si jambo jipya kwa taifa, kwani uchaguzi wa vyama vingi si wa kwanza upo tangu mwaka 1995, na katika kipindi chote hicho haijawahi kushuhudia matatizo makubwa yanayohatarisha amani, huku akiongeza kuwa kwa kuzingatia umoja, mshikamano na uelewa wa watanzania, anaamini uchaguzi wa mwaka huu pia utapita kwa amani kama ilivyokuwa vipindi vyote iliyopita.
Vilevile, Kamanda Senga aliwataka askari hao kuongeza umakini katika kipindi cha uchaguzi na kuhakikisha wanalinda usalama wa wananchi pamoja na mali zao, huku.akisisitiza umuhimu wa kila askari kutimiza haki yake ya kikatiba ya kupiga kura katika vituo watakavyopangiwa, akisema kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya wajibu wao kama raia wa Tanzania.