Na Jeremiah Mbwambo, Dodoma
WAGONJWA wanaofanyiwa upasuaji wa kuondoa mawe kwenye mfumo wa mkojo katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa (BMH) sasa wataruhusiwa kutoka hospitalini ndani ya masaa 24 pekee, badala ya siku tano kama ilivyokuwa awali, kufuatia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya matundu madogo (laparoscopic).
Hayo yamesemwa na Daktari Bingwa wa Mfumo wa Mkojo katika hospitali hiyo, Dkt. Okoa Sukunala, wakati wa kambi maalumu ya matibabu ya kuondoa mawe kwenye mfumo wa mkojo, inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya madaktari bingwa wa BMH na wenzao kutoka Hospitali ya ACIBADEM ya nchini Uturuki.
“Hospitali ya Benjamin Mkapa sasa inatumia vifaa vya kisasa vinavyowezesha kutoa mawe kwenye mfumo wa mkojo bila kufungua mwili. Tunatumia teknolojia ya matundu madogo, ambayo ni salama zaidi na inampunguzia mgonjwa muda wa kupona,” alisema Dkt. Okoa.
Alibainisha kuwa moja ya faida kubwa za teknolojia hiyo ni kupunguza muda wa mgonjwa kukaa wodini.
“Faida ni nyingi, lakini kubwa zaidi ni kwamba baada ya upasuaji huu, mgonjwa hukaa wodini kwa muda usiozidi masaa 24, ikilinganishwa na siku tano tulizokuwa tukitumia hapo awali,” alifafanua Dkt. Okoa.
Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambayo mwaka huu inaadhimisha miaka 10 ya utoaji huduma za afya, imeendelea kuboresha miundombinu na huduma zake, ikijikita zaidi katika matumizi ya teknolojia ya kisasa ya tiba, ikiwemo upasuaji usiohitaji kufungua mwili.
Picha: Jeremiah Mbwambo