Featured Kitaifa

BOT YAKANUSHA KUCHAPISHA FEDHA KUGHARAMIA UCHAGUZI

Written by Alex Sonna

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UPOTOSHAJI WA FEDHA ZINAZOCHAPISHWA NA BENKI  KUU YA TANZANIA PAMOJA NA USHAWISHI WA KUONDOA FEDHA KWENYE MABENKI 

Pamekuwepo na taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Benki Kuu ya Tanzania  kuchapisha fedha na kuzisambaza kwa ajili ya kugharamia uchaguzi; na wengine wakihamasisha  wananchi kuondoa fedha zao kwenye baadhi ya benki za biashara kwa maelezo kuwa benki hizo  zimeishiwa fedha kwa sababu ya uchaguzi. Napenda kuwafahamisha wananchi wote kuwa taarifa  hizo siyo za kweli, zinapaswa kupuuzwa na kukemea wote wanaoupotosha umma kuhusu hali hiyo.  

Benki Kuu ya Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, huchapisha fedha kwa mujibu wa  Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, Sura 197 na kuziingiza kwenye mzunguko kulingana na  shughuli za kiuchumi pamoja na mahitaji ya kubadilisha fedha zinazochakaa pale zinaporejeshwa  Benki Kuu kupitia amana za benki za biashara, na siyo vinginevyo.

Aidha, Benki Kuu imeendelea  kutekeleza vizuri Sera ya Fedha na kuwezesha mfumuko wa bei kuwa wa chini (wastani wa asilimia  3.3 kwa miezi 10 ya mwaka 2025), uchumi kukua kwa kasi (matarajio ya asilimia 6 mwaka 2025),  urari wa malipo nje kupungua hadi asilimia 2.4 ya pato la taifa Septemba 2025; thamani ya shilingi  kuimarika kwa asilimia 8.8 kwa mwaka ulioishia Septemba 2025; na akiba ya fedha za kigeni  kuongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 6.7 zinazokidhi uagizaji wa bidhaa nje kwa miezi 5.4. 

Vile vile, napenda kuwathibitishia kuwa benki zote zilizopo nchini zinasimamiwa kwa kuzingatia  sheria, kanuni, miongozo na vigezo vya kimataifa ambapo zimeendelea kuwa na mitaji ya kutosha,  ukwasi wa kutosha, zinatengeneza faida, na zina kiwango kidogo cha mikopo chechefu (asilimia 3.3  Septemba 2025) ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 5.0. Aidha, mifumo ya malipo inaendelea  kusimamiwa vizuri na kuwezesha miamala yote kufanyika kwa usalama, ufanisi na tija inayostahiki.  

Kutokana na mazingira hayo mazuri ya kiuchumi na kifedha nchini, uamuzi wa kuondoa fedha kutoka  benki na kuzitunza nyumbani haufai kwa kuwa ni utamaduni wa kizamani wenye hatari nyingi ikiwemo  pamoja na kuibiwa, kuvutia wezi wanaoweza kukudhuru, kupotea, kuzitumia vibaya katika shughuli  zisizokusudiwa, kuharibika endapo zitatunzwa vibaya au kuungulia ndani ya nyumba endapo janga  la moto litatokea.

Hivyo, wananchi wanashauriwa kuendelea kutunza amana/fedha zao benki kwa  sababu watapata faida nyingi ikiwemo kulipwa riba au faida ya mwaka, fedha kutunzwa kwa usalama  wa uhakika, kukingwa na bima ya amana muda wote, kuwezesha mabenki kupata fedha za  kukopesha wananchi wanaohitaji mitaji au kukidhi dharura na mahitaji mbalimbali ya kiuchumi. 

Benki Kuu inawasihi wananchi kutokuhamisha fedha zao kutoka kwenye mabenki, bali waendelee kutumia huduma za benki bila wasiwasi wowote.

Vile vile, tunawaonya wote wanaofanya upotoshaji  huo mitandaoni na kuwataka waache kufanya hivyo mara moja, kwani taarifa hizo hazina tija katika  maendeleo ya sekta ya fedha, na uchumi wa Tanzania kwa ujumla.  

About the author

Alex Sonna