Featured Kitaifa

DKT. MWIMANZI AWASISITIZA WATAALAMU KUFUATILIA KANUNI ZA USALAMA WA MIONZI KAZINI

Written by Alex Sonna

 

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Wiki ya mafunzo maalum kwa wataalamu wanaotumia vifaa vya ukaguzi wa mizigo (Baggage Scanners) imehitimishwa kwa mafanikio jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuimarisha usalama wa mionzi katika maeneo ya ukaguzi nchini.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kuanzia Oktoba 6 hadi 10, 2025, yakihusisha wataalamu 31 kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), na kampuni moja ya usambazaji wa vifaa vya ukaguzi wa mizigo.

Mafunzo hayo yalijumuisha mihadhara ya kitaalamu, mijadala ya kina na mafunzo kwa vitendo katika mazingira halisi ya kazi, yakilenga kuongeza uelewa na uwezo wa washiriki katika kutumia teknolojia za ukaguzi kwa usalama zaidi.

Akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat Kassim Mohammed, Mtaalamu wa TAEC Dkt. Jerome Mwimanzi aliwataka washiriki kuendelea kushiriki mafunzo ya aina hiyo mara kwa mara ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha ufuatiliaji wa sheria na kanuni za usalama wa mionzi katika maeneo yao ya kazi.

“Ushiriki wenu unaonyesha dhamira ya kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi. Ni wajibu wetu wote kuhakikisha vifaa hivi vinatumika kwa usalama na kwa kufuata viwango vilivyowekwa,” alisema Dkt. Mwimanzi.

Miongoni mwa mada zilizofundishwa ni Utangulizi wa Mionzi Ionizing, Athari za Kibayolojia za Mionzi, Kanuni za Ulinzi dhidi ya Mionzi, Mfumo wa Kisheria wa Udhibiti wa Mionzi Tanzania, pamoja na Usalama wa Nyuklia na Biashara Haramu ya Vifaa vya Mionzi.

Washiriki walieleza kuridhishwa na mafunzo hayo wakisema yamewapa maarifa mapya kuhusu matumizi salama ya vifaa vya ukaguzi wa mizigo.

“Sasa tunaelewa si tu namna ya kuendesha mashine, bali pia jinsi ya kujilinda na kuwalinda abiria dhidi ya madhara ya mionzi,” alisema mmoja wa washiriki kutoka TPA.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa TAEC wa kuimarisha usimamizi wa usalama wa mionzi nchini na kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanaendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila kuhatarisha afya ya binadamu na mazingira.








About the author

Alex Sonna