Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Katika kujenga utamaduni wa kuheshimu mteja na kuinua viwango vya utoaji huduma nchini, Katibu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juma Mkomi amewaelekeza watumishi kuzingatia wajibu na mamlaka waliyopewa kuhakikisha wanatimiza jukumu la utoaji huduma bora kwa umma kwa misingi ya uadilifu ili kufikia lengo kuu la Serikali.
Katibu Mkuu Mkomi ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 09,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja.
“Ninawaelekeza watumishi wote wa umma katika wiki hii ya huduma kwa mteja, kuzingatia wajibu na mamlaka waliyopewa kwa mujibu wa Katiba hiyo, kuhakikisha wanatekeleza jukumu la utoaji huduma bora kwa umma kwa misingi ya uadilifu, ili kufikia lengo kuu la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 8 (1) (b) ya Katiba, ambalo ni kuleta ustawi wa wananchi,”amesema.
Katika hatua nyingine Mkomi, amewakumbusha Watumishi wote wa Umma kuwa ustawi wa wananchi, utapatikana kupitia utoaji wao wa huduma bora unaozingatia maadili ya utendaji na maadili ya taaluma zao.
“Hivyo wanapotoa huduma kwa wananchi, ni vema wazingatie kuwa nadhifu, waaminifu, wakarimu, wenye heshima, wanaojali utu, wenye kuepuka vitendo vya rushwa, na wenye kujali watu wanaowahudumia,”amewakumbusha.
Amesema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kama Ofisi Simamizi, katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa mteja, tumeendelea kuzingatia misingi ya maadili ya ofisi yetu ambayo ni Uzalendo, Uadilifu, Ubora na Mteja Kwanza, kama sehemu ya kusimamia Dira ya Ofisi inayotutaka kuwa na Utumishi wa Umma wenye ufanisi na uwajibikaji katika kufikia ustawi wa Taifa.
Pia amewaomba watumishi wa umma wote mambo kutumia wiki hii kama chachu ya mabadiliko yao kiutendaji na kujenga taswira chanya kwa wananchi, kwa kuwa utoaji wao wa huduma bora kwa kuzingatia misingi ya maadili utachangia kupunguza malalamiko, kuleta ustawi na kuendelea kujenga imani ya wananachi kwa Serikali yao.
“Pia iwaombe, tupo ndani ya mwezi ambao nchi yetu inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa nafasi za viongozi kwa ngazi ya udiwani, ubunge na uRais, hivyo watumishi wote wa umma watumie haki yao kikatiba wajitokeze siku ya uchaguzi tarehe 29 Oktoba mwaka huu (2025) kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka katika nafasi hizo kwa maslahi ya Taifa hili,”ameomba.
Wiki ya Huduma kwa Mteja Duniani huanza tarehe 6 na kilele chake ni tarehe 10 ya mwezi Oktoba kila mwaka ambapo kupitia maadhimisho haya, taasisi za umma nchini zimekuwa zikishiriki maadhimisho haya, ambayo kwa mwaka huu, yamebeba kaulimbiu isemayo “Dhamira Inayowezekana”.




