……..
Bunge la Afrika Mashariki (EALA) limeeleza kufurahishwa na namna Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) inavyotumia elimu, utafiti na teknolojia kama nyenzo za kuchochea maendeleo endelevu na suluhisho za changamoto za jamii.
Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Jumla wa Bunge hilo, Dkt. Abdullah Makame, alitoa pongezi hizo wakati wa ziara ya wabunge wa EALA katika taasisi hiyo, ambapo walipata nafasi ya kutembelea miradi na bunifu mbalimbali zinazotekelezwa na watafiti wa NM-AIST.
Dkt. Makame alisema mfumo wa elimu wa NM-AIST umejengwa juu ya nguzo tano kuu zinazolenga uhusiano wa karibu kati ya taaluma, utafiti na matumizi yake katika jamii, akisisitiza kuwa ni mfano wa kuigwa kwa taasisi nyingine za elimu ya juu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“NM-AIST imeonyesha kwa vitendo namna sayansi na teknolojia zinavyoweza kuwa injini ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hususan katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Dkt. Makame.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Taasisi anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ubunifu, Prof. Anthony Mshandete, alisema dira ya NM-AIST ni kuhakikisha matokeo ya tafiti yanachangia moja kwa moja katika maendeleo endelevu ya jamii, taifa na bara kwa ujumla.
Aidha, wajumbe wa EALA walitoa mapendekezo kuhusu namna NM-AIST inaweza kuendelea kuimarisha mchango wake katika kufanikisha malengo ya Agenda 2063, dira ya maendeleo ya Afrika yenye ustawi, ushirikishwaji na ubunifu.
Ziara hiyo imeonesha dhamira ya pamoja kati ya EALA na taasisi za elimu ya juu kutumia sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu za kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.
Wakati wa ziara hiyo, wajumbe walitembelea maeneo mbalimbali ya NM-AIST ikiwemo maktaba, maabara, maabara ya akili-tundu (AI Lab), kituo cha TEHAMA, kiwanda kidogo cha DDI, pamoja na Kituo cha Ubunifu cha C-CODE.