Kampeni ya Msaada wa Kisheria inayoratibiwa na kutekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria imefanikiwa kumsaidia Bi. Zulfa Joseph (19) kuachiwa huru baada ya kukaa gerezani kwa mwezi mmoja na wiki moja akiwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu (3).
Bi. Zulfa alipata Msaada wa Kisheria kutoka kwa wataalam wanaotoa huduma za Msaada wa Kisheria katika maeneo ya Magereza na Vizuizi kufika katika Gereza la Butimba Mwanza mnamo tarehe 21 Septemba, 2025 ambapo walimsikiliza na kumsaidia na akafanikiwa kutoka gerezani humo tarehe 25 Septemba 2025.10.
Zulfa alikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi Igoma-Mwanza baada ya kutuhumiwa kumtukana mpangaji mwenzake ambapo yeye amesema mgogoro huo ulitokana na mwanaume huyo kumfuatilia kimapenzi na alipokataa alianza kumpa vitisho na kumtahadhalisha kuwa atapata anachostahili.
“Nilikamatwa tarehe 4 na kupelekwa kituo cha polisi nikawekwa mahabusu kisha kuhamishiwa Nyakato nikiwa na mtoto wangu ambapo nilisomewa shitaka nilikana sikumtukana lakini kwa kukosa msaada mahakamani nilihukumiwa kifungo cha miezi mitatu ama kulipa faini kiasi cha shilingi 500,000’’ alisema Zulfa.
Kutokana na kushindwa kulipa faini hiyo, Zulfa alihamishiwa Gereza la Butimba ambapo alikaa kwa muda wa Mwezi mmoja na wiki moja kabla ya kusaidiwa na wataalam wanaotoa Msaada wa Kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inayotekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria.
“Nimefurahia sana msaada huo, kwa sababu maisha ya gerezani na mtoto mdogo yalikuwa magumu na yalikuwa yananiumiza sana,” amesema kwa hisia.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Bi. Eva Mkonyi amesema kuwa walitembelea Gereza la Butimba kwa lengo la kutoa Msaada wa Kisheria kwa wafungwa na mahabusu walioko katika Magereza 18 zilizoko katika mikoa minne ya Kanda ya Ziwa.
Amesema miongoni mwa wafungwa waliopata Msaada wa Kisheria ni Zulfa, ambaye walimkuta akiwa na mtoto mwenye umri mdogo, hivyo wakaona mazingira ya gerezani hayakuwa rafiki kwa mtoto mdogo ambapo walichukua uamuzi wa kufuatilia kesi yake hadi pale alipofanikiwa kupata haki ya kuachiwa huru.
Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia inatekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kuwasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo, waliopembezoni, na maeneo ya magereza na vizuizi kupata huduma za Msaada wa Kisheria bure ili kuimarisha Upatikanaji wa Haki na Utawala Bora Nchini.