Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Dennis Simba amesema hatua ya kuunganisha Mfumo wa NeST na mifumo ya malipo ya Serikali inayowezesha malipo ya zabuni kulipwa moja kwa moja kupitia Mfumo huo, yatasaidia kupaisha maendeleo ya Taifa.
Bw. Simba ameyasema hayo Oktoba 1, 2025 jijini Arusha, wakati wa kufunga mafunzo ya usimamizi wa mikataba ya ununuzi wa umma hadi kufanya malipo (e-payment) kupitia Mfumo wa NeST, yaliyotolewa na Mamlaka hiyo kwa watumishi wa Ofisi ya Mlipaji Mkuu wa Serikali kwa siku tatu.
Ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mapinduzi chanya kwenye sekta ya ununuzi wa umma.
Amesema Serikali ilifanya mapinduzi kwa kutunga Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kujenga Mfumo wa NeST ambao sasa unawezesha hatua ya usimamizi wa mikataba kidijitali ikiwa ni pamoja na kufanya upekuzi na majadiliano kupitia NeST; na sasa inawezesha kufanya malipo ya zabuni husika kwenye Mfumo huo.
“Kufanya malipo ya zabuni husika kupitia Mfumo wa NeST, kunasaidia kupitia taarifa kamili za zabuni kwenye mnyororo mmoja kwenye Mfumo mmoja.
Hii inatoa nafasi kwa taasisi nunuzi na wazabuni kupata taarifa za malipo kwa wakati, na pande zote mbili zinaweza kujiridhisha kwa kuangalia ukamilishwaji wa kazi na malipo husika bila mzabuni kufuatilia kwenye ofisi za Serikali,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa PPRA.
Amrongeza kuwa hatua hii itasaidia kuondoa changamoto ya malipo yasiyoendana na kazi iliyofanyika, malipo hewa, au kucheleweshwaji wa malipo usio wa lazima. Hivyo, itasaidia kuharakisha maendeleo kwa wananchi.
“Ucheleweshwaji wa michakato ya ununuzi ni sawa na kuchelewesha maendeleo kwa wananchi. Kwahiyo, hatua hii ya Serikali itapaisha maendeleo ya Taifa letu, kwa kuzingatia kuwa zaidi ya 70% ya bajeti ya Serikali inatumika kwenye ununuzi wa umma,” amesisitiza.
Bw. Simba ametoa mfano wa nchi zinazoendelea ambazo zilianza kupaisha uchumi wake baada ya bajeti zao kufikia dola za kimarekani bilioni 20, akilinganisha na wakati huu ambao Tanzania pia imefikisha kiasi hicho cha bajeti na imeanza kufanya mapinduzi makubwa ya kimaendeleo.
Awali, Mhasibu Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bi. Mary Kimambo aliishukuru PPRA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa wahasibu na kuwawezesha kuhudhuria, akieleza kuwa ni nia njema ya kuhakikisha malipo kupitia NeST yanafanyika kwa ufanisi.
Hadi sasa, Mfumo wa NeST ambao umeunganishwa na mifumo zaidi ya ishirini (20), umekamilika katika moduli ya usajili (e-registration), utekelezaji wa zabuni (e-tendering), usimamizi wa mikataba (e-contract) na malipo (e-payment).