: Safari ya mwanamke aliyeleta uhai mpya katika sayansi na uhifadhi.
“RAIS SAMIA AMLILIA”
Katika historia ya utafiti wa Wanyamapori na uhifadhi wa mazingira, huwezi kuacha kutaja jina la Mwanamama Dkt. Jane Goodall. Mwanamke ambaye kwa ujasiri alikanyaga katika misitu ya Gombe iliyopo Mkoani Kigoma nchini Tanzania, akiwa binti mdogo kutoka Uingereza na kuibuka kuwa sauti ya kimataifa kwa wanyamapori, mazingira na kizazi kipya cha watetezi wa maisha na uhai wa wanyamapori hususani Sokwe.
Dkt. Jane Goodall alizaliwa tarehe 3 April, 1934, nchini Uingereza katika familia ya kawaida lakini yenye ndoto kubwa. Safari yake ya kupenda wanyamapori ilianza tangu akiwa binti mdogo kwa kujisomea vitabu kuhusu Afrika na wanyamapori, huku lengo lake likiwa ni kusafiri hadi Afrika na kujifunza zaidi kuhusu maisha wanyamapori.
Mwaka 1960 akiwa na miaka 26 bila mafunzo rasmi ya chuo kikuu, Jane alisafiri hadi Tanganyika (Tanzania) chini ya usaidizi wa mtafiti Louis Leakey. Alianza kazi ya utafiti katika msitu wa Gombe, karibu na ziwa Tanganyika na kufanya uvumbuzi uliobadilisha sayansi ya wanyamapori hususani sokwe na mtazamo wa binadamu kwa viumbe wengine.
Katika hifadhi ya Gombe, alifanya tafiti kadha wa kadha na majaribio mbalimbali kwa kukaa karibu na sokwe, kuvumbua tabia zao bila kuwashambulia na kuandika maelezo ya kila kitendo walichofanya na kuwapa majina kama “David Greybeard”, “Flo” badala ya kutumia namba hatua ambayo ilisukuma mipaka ya mazoea ya utafiti wa kawaida.
Mojawapo ya vumbuzi alizozifanya katika tafiti zake kuhusu maisha ya sokwe ni baada ya kugundua kuwa sokwe hufanya shughuli zao kwa kutumia zana, tabia iliyokuwa ikihusishwa na binadamu pekee hadi wakati huo. Alimwona sokwe akitumia kijiti kuwinda mchwa, jambo lililowalazimisha wanasayansi kuangalia upya tofauti kati binadamu na viumbe wengine. Aidha alithibitisha kuwa sokwe wanahisia, uhusiano wa kifamilia na hulka za kijamii kama ilivyo kwa binadamu. Pia Jane alichagua kuwapa sokwe majina badala ya kuwataja kwa namba kama wanasayansi wengi wafanyavyo.
Baada ya miaka mingi ya utafiti Jane alielekeza nguvu zake katika harakati za kimataifa za uhifadhi wa mazingira. Alianzisha Jane Goodall Institute mwaka 1977, taasisi inayoshirikiana na jamii kulinda makazi ya wanayamapori na kukuza maendeleo endelevu.
Mwaka 1991 alianzisha Roots & Shoots, mpango wa vijana unaowahimiza kuwa viongozi wa mabadiliko chanya katika jamii na mazingira program ambayo imesambaa kwa takribani nchi 100 hivi sasa.
Jane Goodall licha ya kuwa na umri mkubwa bado alikuwa akisafiri duniani kote kuzungumza na watu wa rika zote kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ambapo katika hotuba zake mara nyingi alipenda kutumia maneno yafuatayo:
“Kila mmoja ana nafasi. Kila mmoja wetu ana tofauti. Kila mmoja wetu anaweza kuwa sehemu ya mabadiliko”
Jane Goodall amelala usingizi wa milele lakini jina lake halihusishwi tu na sokwe wa Gombe, bali na mabadiliko ya kimataifa katika jinsi tunavyowatazama wanyamapori, mazingira, na nafasi yetu kama binadamu.
Kwa mujibu wa Jane Goodall Institute, Dkt Jane amefarika dunia akiwa na umri wa miaka 91, kutokana na sababu za asili, akiwa katika ziara yake ya kuzungumza na vijana kuhusu uhifadhi na mazingira huko Califonia nchini Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuma salam zake za rambirambi na kuongeza kuwa “kazi ya Goodall katika hifadhi ya Gombe imefungua milango ya nchi yetu kuwa sehemu ya juhudi za ulimwengu za kutetea mazingira na uhifadhi”
Kufuatia msiba huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana ametoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa uhifadhi kutokana na mchango wake kwa taifa.