Featured Kitaifa

UCSAF YAKAMILISHA MINARA 734, UJENZI WAFIKIA ASILIMIA 96.83.

Written by Alex Sonna

Ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano unaosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefikia hatua kubwa ya mafanikio, ambapo minara 734 tayari imekamilika na inatoa huduma za mawasiliano kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya vijijini nchini.

Hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 96.83, hali inayodhihirisha dhamira ya Serikali kupitia UCSAF kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za mawasiliano, hususan wale wa maeneo ya vijijini na yenye changamoto za kijiografia.

Minara iliyosalia ni 24 pekee, na inatarajiwa kukamilika hivi karibuni ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika katika maeneo yote yaliyopangwa.

Mradi huu ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na kampuni za simu nchini kwa lengo la kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, zikiwemo huduma za intaneti na simu ambazo zimekuwa changamoto katika maeneo yaliyokuwa hayana mtandao wa uhakika.

Wananchi wa vijiji ambavyo minara imekamilika wameshaanza kunufaika na mawasiliano bora, hali ambayo imekuwa chachu ya maendeleo ya biashara, elimu, na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.

Kukamilika kwa ujenzi wa minara yote 758 kutaongeza kasi ya maendeleo ya kidijitali nchini na kufanikisha mpango wa Serikali wa kuhakikisha hakuna mwananchi anayesalia nyuma kutokana na changamoto za mawasiliano.

About the author

Alex Sonna