Featured Kitaifa

MUHIMBILI YAANDIKA REKODI YA KWANZA AFRIKA MASHARIKI, WATOTO 103 WAPANDIKIZWA VIFAA VYA KUSAIDIA KUSIKIA

Written by Alex Sonna

Katika kutekeleza azma ya mageuzi katika sekta ya afya nchini, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeweka historia kwa kuwa taasisi ya kwanza Afrika Mashariki kufanikisha upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia (cochlear implant) kwa watoto 103 ambapo hatua hiyo imeshuhudiwa leo Septemba 29, 2025, baada zoezi la vifaa 16 kuwashwa rasmi kwa watoto waliokuwa wakisumbuliwa na tatizo la kutosikia.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Dkt. Delilah Kimambo, ameeleza kuwa huduma hiyo imewezesha Tanzania kuwa kinara katika ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kutoa huduma hii kupitia hospitali ya umma, jambo ambalo liliwahi kuonekana kuwa ndoto kwa muda mrefu.

“Huduma ya kupandikiza vifaa vya kusaidia kusikia ilianza rasmi nchini Juni 2017 ambapo kabla ya hapo, Serikali ilikuwa inalazimika kuwasafirisha watoto wenye matatizo ya kusikia kwenda nje ya nchi, ambapo gharama ilikuwa takriban shilingi milioni 120 kwa kila mtoto.” ameeleza Dkt. Kimambo.

Tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo nchini, jumla ya watoto 34 walihudumiwa kati ya Juni 2017 na Februari 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 46 kwa kila mtoto, jambo lililoisaidia Serikali kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 ambapo kwa kipindi cha miaka minne chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan watoto 69 wamepandikizwa vifaa hivyo, idadi ambayo ni asilimia 138 watoto ya waliowahi kusafirishwa nje kwa miaka 16 kabla.

“Serikali imetumia shilingi bilioni 3.1 kuwasaidia watoto 69 kupata huduma hii hapa nchini. Kama tungepeleka watoto hao nje, gharama ingefika bilioni 8.2. Hii maana yake ni kwamba tumeokoa zaidi ya bilioni 5 na watoto wengi zaidi wamepata nafasi ya kusikia tena mapema.” amefanunua.

Aidha Dkt. Kimambo ameongeza kuwa siri ya mafanikio hayo ni uwekezaji katika mafunzo ya madaktari wazalendo, ambapo kwa sasa huduma hizo zinatolewa kwa asilimia 100 na wataalamu wa ndani. Vilevile, uwepo wa maabara ya kisasa ya kwanza Afrika Mashariki na Kituo cha Mafunzo ya Upasuaji wa Masikio hospitalini hapo kimeimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha ubobezi barani Afrika, hatua itakayochochea upatikanaji wa huduma endelevu na nafuu zaidi kwa wananchi.

About the author

Alex Sonna